TAMBWE KUIBUKIA YANGA OKTOBA 20

Mshambuliaji mpya wa Simba, Mrundi Amisi Tambwe, 'amewatishia nyau' mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga baada ya kuweka wazi kuwa amejipanga kuwafunga kwenye mechi yao ya kwanza ya ligi kuu itakayopigwa Oktoba 20 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Baada ya kuifungia Simba bao la pili katika mechi waliyotoka sare ya 2-2 dhidi ya Mbeya City, Tambwe alikwenda karibu na jukwaa la mashabiki wa Yanga na kuwanyooshea kidole, ishara ambayo iliibua maswali mengi kutoka kwa watu waliokuwamo uwanjani hapo kushuhudia mchezo huo.

Bao hilo lilikuwa la pili kwa Tambwe katika mchezo huo na la sita kwake kwenye mechi mbili kwani pia alifunga mabao manne wakati Simba ikishinda 6-0 dhidi ya Mgambo Shooting.

Akizungumza katika mahojiano maalum jijini Dar es Salaam juzi, Tambwe alisema aliamua kuwaonyesha ishara hiyo mashabiki wa Yanga kwa sababu walikuwa wakimzomea kabla ya kufumania nyavu.

"Nimejiunga na Simba nikijua kwamba wapinzani wao wakubwa ni Yanga. Walitumia muda wao kunizomea kabla ya kufunga. Na hata nilipofunga bao la kwanza waliendelea kunizomea. Najipanga kuhakikisha ninaifunga timu hiyo tutakapocheza nayo," alisema Tambwe.

Mrundi huyo aliyetua Simba msimu huu baada ya kuipa Klabu ya Vital'O ubingwa wa Ligi Kuu Burundi pamoja na Kombe la Kagame, kwa sasa anaongoza kwa ufungaji katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara akiwa na mabao sita.

Tambwe, ambaye amecheza dakika zote 360 katika mechi nne ambazo vinara wa msimamo huo, Simba walizocheza dhidi ya Oljoro JKT, Mtibwa Sugar, Mgambo na Mbeya City, hakufunga katika mechi mbili mfululizo.

Mechi ambazo hakufunga ni wakati wakishinda 1-0 ugenini dhidi ya Oljoro JKT na 2-0 nyumbani dhidi ya mabingwa wa 1999 na 2000 Mtibwa Sugar.

Kadhalika Tambwe ambaye ni mfungaji bora wa Kombe la Kagame msimu huu, hakucheza mechi ya ufunguzi waliyong'ang'aniwa kwa sare ya 2-2 dhidi ya Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora baada ya yeye na Mrundi mwenzake, Gilbert Kaze kuzuiwa na Shirikisho la Soka nchini(TFF) kutokana na kuchelewa hati zao za Uhamisho wa Kimataifa (ITC).

Msimu uliopita katika Ligi Kuu ya Burundi, Tambwe aliibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao 21 katika mechi 18, na baadaye kufanya hivyo tena kwa kufumania nyavu mara sita kwenye michuano ya Kombe la Kagame iliyofanyika mjini Darfur, Sudan na Vital'O kutwaa ubingwa.

Mrundi huyo anatajwa kuwa mrithi sahihi wa Mganda Emmanuel Okwi ambaye aliuzwa kwa Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia msimu uliopita, jambo ambalo lilichangia Simba kupoteza ubingwa kwa mahasimu wao wa jadi, Yanga.

Okwi na benchi la Ufundi la Yanga likiongozwa na kocha wao, Mholanzi Ernie Brandts walikuwapo uwanjani Jumamosi wakati Tambwe akidhihirisha makali yake kwa kufunga mabao mawili kwenye mechi hiyo.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA