SIMBA YAINGIA MCHECHETO, YATISHWA NA KASI YA MBEYA CITY

Timu ya Mbeya City ambayo imepanda daraja la ligi kuu ya Bara kwa mara ya kwanza katika historia yake mwaka huu inaweza kuwa inalingana kwa pointi na mabingwa watetezi Yanga ambao waliilazimisha kutoka sare ya 1-1 wiki iliyopita, lakini inakutana na mtihani wake mgumu zaidi leo itakapokuwa mgeni wa Simba kwenye Uwanja wa Taifa.


Tangu ianze kucheza kwa mara ya kwanza ligi kuu mechi nne zilizopita, City haijafungwa ikiwa na pointi sita zilizotokana na sare tatu na ushindi katika mchezo mmoja -- kama Yanga.

Lakini inaikabili Simba leo katika mchezo wake wa pili tu ugenini huku mabingwa hao wa mwaka jana wakiwa wenye ari kubwa iliyotokana na ushindi mkubwa wa mabao 6-0 dhidi ya Mgambo JKT kwenye uwanja huo, katikati ya wiki.

Kupata ushindi mkubwa zaidi katika msimu huku mshambuliaji wake tegemeo Amisi Tambwe akifikia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika mechi moja ya ligi kuu ni mazingira ambayo yangeweza kuifanya Simba ipoteze umakini inapokutana na City.

Lakini bahati mbaya kwa wageni hao wa ligi kuu, kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu amesema timu yake haijabweteka kwa ushindi wake wa kishindo.

Akizungumza jana, Kihwelu alisema hata kuifunga Mgambo hakujawathibitishia kuwa wana kikosi bora kuliko timu nyingine kwenye ligi hiyo, ikiwemo City, hivyo wataikabili kwa uzito sawa na mechi nyingine.

"Sisi tunaendelea kujipanga, kama benchi la ufundi kila mchezo kwetu tunauchukulia katika uzito sawa bila kuangalia tunacheza na nani," alisema.

"Tumejiandaa kuwakabili kwa nguvu zote Mbeya City kwa sababu ni moja ya timu nzuri kwenye ligi. Hatutawadharau kamwe."

Alisema anaifahamu City kama timu yenye kikosi kilichokaa pamoja kwa muda mrefu na hivyo matokeo inayopata hayamshangazi.

Mbali na sare dhidi ya Yanga, City ilipata matokeo hayo dhidi ya Kagera Sugar na Coastal Union na kuifunga Ruvu Shooting 2-1.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA