MAKALA: SUGU, KAIMBE MUZIKI, MJENGONI HAKUKUFAI.........
Makaburu waliendesha kampeni yao ya ubaguzi wa rangi iliyopelekea mauaji kwa wazalendo wa nchi hiyo ambao wengi wao walikuwa watu weusi, walibaguliwa vya kutosha.
Muziki wa reggae ulitumika kama sehemu ya kufikisha ujumbe kwamba wazalendo wanateseka na sasa waachiwe huru, Mwaka 1990 Nelson Mandela aliruhusiwa kutoka kifungoni ambapo alihukumiwa kwenda jela maisha ili kuwatetea wazalendo.
Baadae Afrika Kusini ikawa huru, safari za Watanzania kwenda `Sauzi`au Bondeni kama wanavyoita zikaanza kuongezeka lakini ukitaja orodha ya wanaharakati wa ukweli waliojitoa kwa nguvu zao hadi kupatikana uhuru kamili Lucky Dube ni miongoni mwao.
Orodha hiyo pia inawataja Miriamu Makeba,Ivonne Chakachaka na wengineo wengi ambao wanaeshimika, lakini cha kushangaza wote hao hawakuwahi kuthubutu kugombea ubunge wala udiwani.
Wameishia kuimba muziki na heshima wakaipata tena ulimwengu mzima unawatambua, Tanzania haikupitia shuruba kama ilizopitia Afrika Kusini,labda Watanzania waliduwazwa kwa kunyimwa Elimu, maana wakati wa Baba wa Taifa marehemu Mwl Julias Kambarage Nyerere akienda UN kuomba uhuru, nchi yetu ilikuwa na wasomi 7 tu.
Kwa sasa nchi yetu tayari iko huru, fulsa tu ndizo zinazohitajika kutumiwa vema lakini kuna kundi kubwa la watu wanaojiita wanaharakati tena wana misimamo mikali.
Joseph Mbilinyi a k a Sugu au Mr 11 ni miongoni mwa wanaharakati waliopo hapa nchini, Sugu alianza kujiingiza kwenye harakati pale alipoanza kuimba muziki wa kufokafoka maarufu Rap.
Muziki huo ulianza kushamili hapa nchini katika miaka ya 90 ambapo vijana wengi walikita, licha kwamba ulionekana wa kihuni lakini ukaja kukubalika ndipo Mr 11 alipoanza kung'ara.
Ingawa katika tungo zake hakuwahi kuipinga serikali wala kuonyesha hisia kwamba ni mwanaharakati, isipokuwa ameonekana kama mwanaharakati kutokana na hisia zake.
Tungo zake nyingi ziliusiana na mapenzi, majisifu nakufurahi, Aliyekuja kuonekana mwanaharakati wa waziwazi ni msanii mwenzake Joseph Haule`Profesa Jay`.
Jay aliimba nyimbo zilizonyesha kupinga baadhi ya tabia za wanasiasa ambao huomba kura ili kuongoza kwa kusema uongo, Lakini Sugu ndiye msanii aliyepata mafanikio pengine kuliko msanii yeyote hapa nchini.
Aliweza kufyatua album tano mfululizo na enzi yake hakuwa na mshindani, ziara yake nchini Marekani ilianza kumjenga zaidi na kuitangaza Tanzania kimataifa.
Akiwa Marekani Sugu alizindua album yake ya sita iliyojulikana kwa jina la 'Deiwaka', baadae alikuja na mipango mizuri ya kuanzisha kampuni yake ya kusaidia wanamuziki chipukizi.
Kampuni hiyo ilifahamika kwa jina la 'Deiwaka Production' ambapo pia ilikuwa na wazo la kuanzisah kampeni ya kupambana na malaria iliyofahamika kwa 'Malaria haikubaliki' ambayo baadaye ilileta kizaazaa baina yake na Cloud`s Media iliyopo chini ya Joseph Kusaga na Ruge Mutahaba.
Sitaki kuelezea ugomvi wake na Ruge kwani walifikia pabaya mpaka nyimbo za matusi zilitungwa, Ila Sugu akajitosa rasmi kwenye harakati za kutaka kuking'oa chama tawala madarakani.
Sugu alijiingiza kwenye ulingo wa siasa na akajiunga na chama chenye ushawishi mkubwa wa nguvu ya umma (CHADEMA) na moja kwa moja akateuliwa kluwa mgombea ubunge Mbeya mjini.
Chama hicho kwa kutambua heshima aliyonayo Sugu kwenye muziki kama ilivyo kwa Lucky Dube wa Afrika Kusini ikamkabidhi jimbo la Mbeya mjini kuwania Ubunge.
Hakupata upinzani akafanikiwa kumbwaga mpinzani wake ambaye alikuwa mwanachama wa chama tawala CCM, kwa heshima aliyonayo Sugu ni lazima apate ushindi, Sugu ndiyo aliemuinua kimuziki Afande Sele, Stara Thomas na Lady Jay Dee si mtu wa masihara hata kidogo.
Lakini alipofanikiwa kuingia 'Mjengoni' ameshindwa kung'ara kama alivyokuwa aking'ara kwenye muziki.
Sijaona makali ya Sugu kwenye pale 'mjengoni' kama ilivyokuwa kwenye muziki, cha zaidi nimeona fedheha dharau kwa mheshimiwa huyo nilimuhusudu sana enzi za `Mambo ya fedha, Dar DSM na Deiwaka.
Sugu amedhalilishwa mno pale kikosi cha usalama bungeni walivyotumia maguvu yao kumkwida na kumpiga kama kibaka au mtumiaji wa dawa za kulevya`Teja.
Heshima yote aliyokuwa nayo na uheshimiwa wake kutokana na siasa ilikuwa kazi bure. Nikiwa kama shabiki wake kwenye muziki namuomba arejee kwenye tasnia yake ya muziki, kule `Mjengoni akumfai.
Tanzania tunafanya siasa baridi hakuna haja ya kugombana kama ilivyotokea hivi karibuni ambapo wabunge wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kuzichapa kavukavu. Tuonane wiki ijayo.