ANGALIA JINSI AMRI KIEMBA ANAVYOFANANISHWA NA MESSI

KIUNGO tegemeo wa Simba SC, Amri Ramadhani Kiemba amepata ugonjwa sawa na ambao unamuweka nje Mwanasoka Bora wa Dunia, Lionel Messi kwa wiki tatu, huo si mwingine ni maumivu ya nyama.


Tofauti tu ni kwamba, Muargentina wa Barcelona ya Hispania, Messi maumivu yake ni ya mguu wa kulia, wakati Kiemba ni mguu wa kushoto.
Kiemba aliumia jana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC ikishinda mabao 2-0 dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Lakini Kiemba aliyewahi kuchezea Kagera Sugar ya Bukoba, Yanga SC ya Dar es Salaam na Miembeni ya Zanzibar alisema hatarajii kama maumivu yake yatamuweka nje muda mrefu kama Messi.

“Mimi sihisi maumivu sana, ni kidogo tu, ngoja nijisikilizie siku moja na pia nitasikiliza ushauri wa Daktari, baada ya hapo nitajua itakuwa ni muda gani,”alisema Kiemba jana baada ya kuulizwa kuhusu hali yake.

Simba SC ilipata pigo dakika ya 30 tu jana, baada ya kiungo wake huyo mwenye rasta na muumini safi wa dini ya Kiislamu, Kiemba kuumia na kutoka nje, nafasi yake ikichukuliwa na Ramadhani Singano ‘Messi’, aliyekwenda kufunga bao la pili.

Katika mchezo huo, hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Mrundi Amisi Tambwe dakika ya 24 kwa penalti, baada ya beki Jamal Said wa JKT Ruvu kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.

Kipindi cha pili, Simba SC walikianza kwa kasi na kufanikiwa bao la pili dakika nne tu tangu kuanza kwa ngwe hiyo ya lala salama kupitia kwa Messi wa Msimbazi.

Messi alifunga bao hilo baada ya kuuwahi mpira uliorudishwa na mabeki wa Ruvu kufuatia Amisi Tambwe kuunganisha krosi maridadi ya Abdulhalim Humud ‘Gaucho’.
Kwa matokeo hayo, Simba SC inatimiza pointi 14 baada ya kucheza mechi sita na kujiimarisha kileleni mwa ligi hiyo.

Lionel Messi ataikosa mechi ya kesho ya Ligi ya Mabingwa Kundi H ugenini dhidi ya Celtic ya Scotland, na kuwa nje kwa wiki tatu nyingine, baada ya kuumia nyama za mguu wake wa kulia.

Mwanasoka huyo bora wa dunia alitolewa wakati timu yake ikhinda 2-0 dhidi ya Almeria Jumamosi muda mfupi tu baada ya kufunga bao la kwanza dakika ya 21, ambalo lilikuwa bao lake la nane msimu huu.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA