YANGA MATAWI YA JUU, YAI[A KIPIGO CHA MBWA MWIZI ASHANTI
Mabingwa watetezi Yanga jana walitumia vizuri ugeni kwenye ligi kuu
ya Bara wa Ashanti United iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani kufunga
mabao matatu ya mapema katika kila kipindi, yaliyoisaidia kuichabanga
5-1 na kuipa pointi tatu baada ya mchezo mmoja.
Ashanti ilimaliza mchezo huo ikiwa na
wachezaji 10 baada ya Emmanuel Kichiba kutolewa uwanjani na muamuzi
Israel Nkongo kwa kosa la pili la kadi ya njano katika robo saa ya
mwisho.
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts alisema
alitaraji kiwango cha ushindi ambacho timu yake ilipata kwa sababu
aliingiza timu uwanjani akiwa haidharau Ashanti kutokana na kutoifahamu.
Mwalimu wa Ashanti, Hassan Banyai alisema
timu yake ilizidiwa kwa sababu ya kuwa na wachezaji wengi wageni
kulinganisha na Yanga ambayo ni timu kubwa iliyocheza pamoja kwa muda
mrefu.
Nizar Khalfani na Haruna Niyonzima
waliifungia Yanga mabao la nne na tano ya mwishoni mwa mchezo, moja
katika dakika ya 90, lakini kuchabangwa huko kwa Ashanti kwenye ligi
kulijengwa mwanzoni mwa vipindi viwili vya mchezo huo kwenye Uwanja wa
Taifa.
Ikionyesha dhahiri mchecheto wa kurudi kwa
mara ya kwanza kwenye ligi hiyo ya hadhi ya juu zaidi nchini, Ashanti
iliyokuwa na jezi za rangi ya machungwa na bukta nyeusi haikuwa imetulia
hivyo kutoa mwanya kwa Yanga kutawala uwanjani katika dakika 15 za
kwanza.
Haikushangaza basi kuona Jerry Tegete
akiipatia bao la kwanza kutokana na pasi fupi ya Simon Msuva katika
dakika ya 10 baada ya mshambuliaji huyo kumzunguka beki wa Ashanti,
Tumba Sued, na kuutumbukiza mpira wavuni kirahisi.
Bao la Tegete lilikuja dakika moja tangu
Mussa Kanyaga ashindwe kuifungia Ashanti bao la wazi alipompa mpira
mikononi Ally Mustafa katika lango la Yanga, baada ya kumtoka Nadir
Haroub.
Ashanti ambayo ilielekea haikujifunza
kutokana na makosa ya dakika za mwanzoni za kipindi cha kwanza,
ilijikuta ikifungwa mabao mawili ya haraka ndani ya dakika 12 za kwanza
za kipindi cha pili pia.
Mpishi wa bao la kwanza Msuva aliifungia
Yanga goli la pili dakika mbili tangu kuanza kwa ngwe ya pili, baada ya
kupiga shuti la mbali lililokwenda moja kwa moja wavuni.
Ilimchukua Tegete dakika 10 zaidi
kuifungia Yanga bao ambalo lilimaliza ushindani wa mechi hiyo na
kuihakikishia Yanga mwanzo mzuri wa msimu mpya, aliposhirikiana tena na
Msuva kutumbukiza mpira wavuni.
Khalfani aliifungia Yanga bao la tano
katika dakika ya mwisho ya mchezo kutokana na pasi ya Domayo wakati
Niyonzima aliifungia bao la nne zikiwa zimebaki dakika 17 mpira
kumalizika.
Bao la kupoza machungu kwa Ashanti lilifungwa na Shaban Juma aliyeingia kutoka benchi, dakika moja kabla ya goli la Khalfani.
Timu zilikuwa:
YANGA: Ally Mustafa, Juma Abdul, David
Luhende, Nadir Haroub, Mbuyu Twite, Athumani Iddi (Frank Damayo dk.18),
Simon Msuva, Salum Telela, Didier Kavumbagu, Jerry Tegete (Nizar
Khalfani dk.81), Haruna Niyonzima.
ASHANTI: Ibrahim Abdallah, Khan Usimba,
Emmanuel Kichiba, Ramadhani Malima, Tumba Sued, Emmanuel Memba, Fakihi
Hakika, Mussa Nampaka (Laurent Mugia dk.61), Hussein Sued, Musa Kanyaga,
Joseph Mahundi (Hussein Mkongo dk.84).