SIMBA YAUMBULIWA NA RHINO, PENGO LA KASEJA LAONEKANA
Simba jana ilianza kwa lawama na majanga msimu mpya wa ligi kuu ya
Bara baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na timu ya Rhino Rangers
iliyopanda daraja kwa mara ya kwanza na ambayo Wekundu wa Msimbazi
walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuifunga.
Mara baada ya pambano hilo kwenye Uwanja
wa Ali Hassan Mwinyi hapa, kocha wa Simba Abdallah Kibadeni alisema
matokeo hayo yamesababishwa na Abel Dhaira kufungwa magoli ya kizembe
langoni mwa timu hiyo ya Msimbazi.
Saddy Kipanga ndiye aliyeifungia Rhino bao
la kusawazisha dakika 25 kabla ya filimbi ya mwisho kwa shuti kali la
mpira wa adhabu ndogo kutoka mita 20, ambalo lilimpita ubavuni Dhaira
katika lango la Simba.
Adhabu ndogo hiyo ilikuwa imetolewa na
muamuzi Amon Paul baada ya Issa Rashid 'Baba Ubaya' kumkwatua mchezaji
wa zamani wa Simba Nurdin Bakari nje kidogo ya eneo la hatari.
Bao hilo liliamsha shangwe za watazamaji
takribani 20,000 waliohudhuria mechi ya kwanza ya ligi kuu ya Bara mjini
Tabora katika miaka 14, tangu Milambo iliposhuka daraja 1999.
Jonas Mkude aliifungia Simba bao la kwanza
katika dakika ya 12 kwa kichwa kutokana na mpira wa kona iliyopigwa na
'Baba Ubaya' na kuweka matumaini ya kufanya kile ambacho wachambuzi wa
soka walitaraji.
Lakini ndoto hiyo ilianza kuingia dosari
dakika nane kabla ya mapumziko, wakati Iman Noel alipoifungia Rhino bao
la kwanza kwa mpira wa adhabu ndogo kutoka nje kidogo ya eneo la hatari.
Adhabu hiyo ambayo ilimshinda Dhaira kwa
staili ile ile ya goli la pili la wenyeji, ilitolewa baada ya beki
Mirani Athumani wa Simba kumrukia mgongoni Victor Hangaya.
Mkude aliifungia Simba bao la pili katika
dakika ya 41 baada ya muamuzi Paul kuamuru tuta hilo kutokana na
Stanslaus Mwakitosi kumuangusha Amri Kiemba ndani ya 18.
Timu zilikuwa:
RHINO: Abdulkarim Mtumwa,
Ally Ahmed, Hussein Abdallah, Julius Masunga, Laban Kambole, Stanslaus
Mwakitosi, Daniel Manyenya (abbas Mohammed dk.66), Iman Noel, Victor
Hangaya, Nurdin Bakari, Sady Kipanga.
SIMBA: Abel Dharia,
Nassoro Masoud, Issa Rashid, Miraji Adam, Joseph Owino, Jonas Mkude,
Ramadhani Chombo (Ramadhani Singano dk.62), Ndemla Said, Amri Kiemba,
Betram Mwombeki (William Lucian dk.36), Haruna Chanongo.