SIMBA KAMILI GADO KUIVAA JKT OLJORO, TAMBWE, KAZE YAWAPA JEURI



Baada ya uongozi wa Simba kufanikiwa kupata Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) za nyota wao wa kigeni Warundi, Amisi Tambwe na Gilbert Kaze, meneja wa timu hiyo, Mosses Basena (Pichani) amesema kikosi chao sasa ni ‘moto wa kuotea mbali’.


Akizungumza jana akiwa Arusha, Basena alisema anaamini nyota hao watakisaidia kikosi cha ‘Wanamsimbazi’ kilicholazimishwa sare ya 2-2 dhidi ya ‘maafande’ wa Rhino Rangers katika mechi yao ya ufunguzi wa msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora Jumamosi.

“Tunashukuru Mungu tulifika salama Arusha jana (juzi) saa mbili usiku. Tumefarijika kupata ITC za wachezaji wetu (Tambwe na Kaze) ambao walizuiwa kucheza Tabora,” alisema Basena.

“Tambwe na Kaze ni wachezaji wazuri. Naamini wataiimarisha timu yetu. Kikosi chetu sasa kimekuwa moto na hatuna wasiwasi wa kufanya vibaya katika mechi zijazo,” aliongeza Mganda huyo.

Mshambuliaji Tambwe na beki wa kati Kaze, ambao walilazimika kuwa watazamaji katika mechi ya Jumamosi baada ya Shirikisho la Soka (TFF) kuwazuia kucheza kutokana na kutokuwa na ITC, wameingia mikataba ya miaka miwili na Simba wakitokea klabu ya Vital’O ya Burundi, waliyoipa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) mwaka huu.

Katika mashindano hayo ya Kombe la Kagame, ambao mwaka huu timu za Simba, Yanga na Super Falcon za Tanzania hazikushiriki kwa hofu ya usalama wa nchini Sudan, ambako mashindano hayo yalifanyika, Tambwe aliibuka mfungaji bora.

Kabla ya kutua Simba, Tambwe pia aliifungia Vita’O magoli 21 katika mechi 18 za msimu huu wa Ligi Kuu ya Burundi, na ndiye anaongoza kwa magoli katika ligi hiyo.

Aidha, Basena ambaye aliwahi kuwa kocha wa Simba, alisema kikosi chao kinaendelea vyema na maandalizi ya mechi yao ya pili ya ligi hiyo dhidi ya Oljoro JKT itakayopigwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kesho.

“Mechi ya Jumatano (kesho) itakuwa ngumu ukizingatia wapinzani wetu wako nyumbani na walipoteza mechi yao ya kwanza Jumamosi,” alisema.

Oljoro JKT ilianza vibaya msimu huu baada ya kulala 2-0 nyumbani dhidi ya mabingwa wa mwaka 1988 wa Tanzania Bara, Coastal Union katika mechi yao ya ufunguzi wa msimu huu kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Jumamosi.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA