ROMA MKATOLIKI AFANYA MAKAMUZI YA HATARI DAR

Msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya, Roma Mkatoliki na bendi ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twnaga Pepeta' walikonga nyoyo za mashabiki tele waliojitokeza katika bonanza maalum lililoandaliwa kwa udhamini wa kinywaji cha Vita Malt kwenye viwanja vya Posta, Kijitonayama jijini Dar es Salaam juzi.


Roma Mkatoliki alipagawisha watu zaidi kutokana na vibao vyake vikali kama 'Tanzania' na 'Mathematics', huku mashabiki wakimshangilia zaidi kutokana na namna alivyokuwa akighani mashairi yake kwa hisia kali.

Kiongozi wa Twanga Pepeta, Luiza Mbutu, alishirikiana na wenzake katika kunogesha zaidi bonanza hilo kutokana na uimbaji wao na kucheza kwa kujituma kuanzia mwanzo hadi mwisho, hivyo kuwa kivutio kwa kila aliyehudhuria.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa bonanza hilo, Meneja wa Vinywaji visivyo na Vileo katika Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Consolata Adam, alisema kuwa  waliamua kuandaa tamasha hilo kwa nia ya kuwakutanisha pamoja wafanya mazoezi wote kutoka katika vituo maalumu (gym).

“Tuliamua kuandaa bonanza linalowakutanisha wanamichezo mbalimbali, hasa wafanya mazoezi ili wajumuike pamoja katika kufanya mazoezi," alisema, akiongeza kuwa wanamichezo kutoka katika vituo 10 vya gym walishiriki bonanza hilo, wakiongozwa na wakufunzi kumi ambao waliongozwa na mkufunzi wa kimataifa Shadrack Opulukwa.

Alizitaja gym zilizoshiriki kuwa ni Better Life, Genessis ya Kijitonyama, Segerea Gym, Rio Gym, Genessis ya Kimara, Azula ya Mikocheni na Serena Gym.

Kivutio kikubwa katika bonanza hilo ilikuwa ni ushindani kutokana kwa baa za Fyatanga ya Tegeta na Kisuma ya Temeke, ambazo zilionyeshana umwamba katika kuandaa nyama bomba.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa TBL, Edith Mushi, alisema wanashukuru kwa kiasi kikubwa kufanikiwa kwa bonanza hilo kwani wamesaidia pia kujenga afya za Watanzania.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA