MPINZANI WA CHEKA KUTUA DAR, MASHALI KUOGOPA MZIKI WA MAUGO
Wakati bondia Phil Williams kutoka Marekani pamoja na kocha na daktari wake wanatarajia kutua nchini usiku wa leo ili kumkabili Francis Cheka, bondia Thomas Mashali ameendelea kusisitiza kuwa hatapigana na Mada Maugo siku ya Ijumaa.
Cheka na Williams wanatarajiwa kupigana kuwania ubingwa wa kimataifa wa WBF katika pambano la uzani wa Super Middle raundi 12 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam siku ya Agosti 30.
Rais wa TPBO-Limited wanaosimamia pambano hilo na mengine ya utangulizi siku hiyo, Yasin Abdallah 'Ustaadh' alisema usiku wa jana walituma tiketi ya bondia huyo na wasaidizi wake na watatua nchini leo saa 3:50 usiku.
Ustaadh alisema kutua kwa Mmarekani huyo ni uthibitisho kwamba maandalizi ya pambano hilo yamepamba moto huku akiwaonya mashabiki na mabondia wasio na nidhamu kujihadhari mapema siku ya pambano kwa ulinzi utakuwa mkali.
"Bondia wa Marekani Phil Williams atatua nchini saa 3:50 usiku wa kesho (leo) akiwa na kocha wake, Filbert Songola na daktari aitwaye Charles na TPBO-Limited tunawaonya mashabiki kujiepusha na uhuni siku ya pambano," alisema.
Alisema onyo hilo wanalitoa mapema kutokana na ukweli kwamba mapambano hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na mabalozi, mawaziri na viongozi wenye heshima zao na kwamba ulinzi utakuwa mkali hiyo asingependa wachache kuwavurugia.
Katika hatua nyingine bondia Thomas Mashali ameendelea kusisitiza kuwa hatapanda ulingoni Ijumaa kuzipiga na Mada Maugo akisema halitambui pambano hilo.