LIGI KUU BARA YAANZA KWA KISHINDO, MABAO 19 YAFUNGWA
Idadi hiyo ya mabao ni kubwa zaidi ukilinganisha
na ile iliyopatikana katika mechi za ufunguzi msimu uliyopita, ambapo
mabao 10 pekee yalifungwa.
Katika ufunguzi huo, kiungo wa Mtibwa Sugar, Juma
Luzio alijiandikia rekodi yake binafsi baada ya kuwa mchezaji wa kwanza
kufunga bao la kwanza na la mapema zaidi msimu huu.
Luzio alifunga bao lake
hilo dakika ya pili ya mchezo kati ya Mtibwa na Azam FC uliopigwa
kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mshambuliaji wa Yanga, Jerryson Tegete na kiungo
wa Simba, Jonas Mkude waliuanza msimu mpya kwa kishindo baada ya kila
mmoja kupachika mabao mawili, idadi ambayo ndiyo ya juu zaidi kwa
mchezaji mmoja mmoja katika mechi hizo za ufunguzi.
Tegete alionyesha makali hayo wakati Yanga
ilipoisambaratisha Ashanti United kwa jumla ya mabao 5-1, wakati Mkude
aliisaidia Simbakulazimisha sare ya mabao 2-2 na Rhino FC ya Tabora.
Mabeki waliojifunga wakiwa katika harakati za
kuokoa hatari langoni mwao ni Laurian Mpalile wa Prisons ya Mbeya katika
mechi dhidi ya Ruvu Shooting wakati timu yake ilipolala mabao 3-0, na
Yusuph Machogote wa Oljoro JKT wakati timu yake ilipochapwa na Coastal Union mabao 2-0.
Pia, waamuzi walitoa kadi mbili nyekundu na mikwaju mitatu ya penalti katika baadhi ya mechi hizo za ufunguzi.
Nyota waliokumbana na rungu la kulimwa kadi nyekundu ni Malegesi Mwangwa wa Kagera Sugar na Emmanuel Kichiba wa Ashanti United.
Kwa upande wa penalti, Aggrey Morris wa Azam FC na
Jonas Mkude wa Simba walizifungia timu zao penalti huku zikitoka sare
wakati beki Stanley Nkomola wa
JKT Ruvu akikosa mkwaju wake, baada ya kupaisha juu ya lango la Mgambo
JKT iliyokubali kichapo cha mabao 2-0 nyumbani.
Hata hivyo, katika viwanja saba vilivyokuwa
vikiwaka moto, Uwanja wa Sokoine Mbeya ndiyo pekee mashabiki wake
walishindwa kushuhudia bao baada ya Kagera Sugar kuwalazimisha suluhu ya
0-0 wenyeji Mbeya City.