HENRY JOSEPH SHINDIKA KUTAMBULISHWA SIMBA JUMAPILI

KOCHA Mkuu nwa Simba SC, Alhaj Abdallah ‘King Kibaden’ amelainika kwa Mwenyekiti wa klabu yake, Alhaj mwenzake, Ismail Aden Rage na kukubali timu hiyo icheze mchezo wa kirafiki Jumapili Dar es Salaam na Mafunzo ya Zanzibar.


Mchezo huo ni maalum kuwatambulisha wachezaji wapya wa Simba SC, Warundi, beki Kaze Gilbert na mshambuliaji Tambwe Amisi baada ya kupatiwa Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC).

Mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, pia utatumika kumtambulisha kiungo Henry Joseph (Pichani) aliyesajiliwa tena Simba SC akitokea Kongsvinger ya Norway ambako alikwenda mwaka 2009 akitokea kwa Wekundu hao wa Msimbazi baada ya kupiga kazi tangu mwaka 2005

Awali, Kibadeni alikataa timu kucheza mechi hiyo na akasema icheze Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya mchezo wa jana wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania na JKT Oljoro, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, ambao Simba ilishinda 1-0, bao pekee la Haroun Athumani Chanongo dakika ya 34.

Lakini baada ya ‘wakubwa’ hao kuzungumza wameafikiana na sasa Wekundu wa Msimbazi watakipiga na Mafunzo Jumapili Taifa na Mwandaaji wa mchezo huo, George Wakuganda amesema maandalizi yanaendelea vizuri na wana Simba watarajie burudani muruwa siku hiyo.

Mwenyekiti huyo wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage alilazimika kwenda Burundi kufuata ITC za wachezaji hao mwishoni mwa wiki baada ya kuona zinachelewa kufika nchini, hivyo kuwachelewesha pia kuanza kazi.

Rage aliondoka Dar es Salaam Jumamosi usiku na ndani ya saa 24 alifanikisha suala hilo na hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Rage, ambaye ana uzoefu wa kuongoza soka kwa zaidi ya miongo mitatu, kuingilia kati suala la uhamisho wa wachezaji wa kimataifa na kufanikisha baada ya miaka miwili iliyopita, kusafiri hadi Jamhuri ya Afrika ya Kati kushughulikia ITC ya mchezaji Gervais Kago ambao nao ulikuwa na matatizo.

Baada ya kupata ITC hizo, Kaze na Tambwe walianza kazi rasmi jana Simba SC katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya JKT OIjoro ya Arusha jana mjini Arusha na kuchangia ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu. Simba tayari imewakatia wachezaji hao vibali vya kufanya kazi hapa nchini.

Wachezaji wengine wa kigeni wa Simba, Waganda Joseph Owino na Abel Dhaira, wamecheza mechi zote mbili za awali za Ligi Kuu, kutokana na kukamilishiwa taratibu zote za uhamisho na kuwa na vibali vya kufanya kazi hapa nchini.

Kaze na Tambwe waliosajiliwa kutoka mabingwa wapya wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Vital’O ya kwao, Jumamosi walikuwapo Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora kuishuhudia timu yao ikilazimishwa sare ya 2-2 na Rhino katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA