CHEKA NA MMAREKANI WAKE KUPIMA UZITO LEO



Mabondia Francis Cheka (Pichani) kutoka Morogoro na Phil William wa Marekani wanatarajia kupima uzito leo kujiandaa na pambano la kuwania ubingwa wa Shirikisho la Ngumi la Dunia (WBU) litakalofanyika kesho kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.


Katika mapambano ya siku hiyo yaliyoandaliwa na Hall Fame Boxing & Promotions yaliyopewa jina la'Usiku wa ubingwa Tanzania', Cheka ambaye ni bingwa wa Afrika wa IBF mwenye rekodi ya 28-7 KO 6, atavaana na mpinzani wake William kutoka Jimbo la Minneapolis, Minnesota Marekani mwenye rekodi ya 12-5 KO 11.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, mratibu wa pambano hilo kutoka kampuni ya Hall of Fame, Jay Msangi, alisema kuwa maandalizi yamekamilika kama walivyopanga ikiwa ni pamoja na kuwasili kwa mabondia kutoka Marekani.

Msangi alisema kuwa mabondia watapima uzito leo saa 3:00 asubuhi kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo).

Alisema kabla ya pambano kuu la kina Cheka kutakuwa pia na pambano jingine la raundi 12 kuwania mkanda wa Afrika uzito wa 'super middle' ambapo Mada Maugo (15-9, KO 11) aliye namba tatu kwa ubora nchini anatarajiwa kupambana na Thomas Mashali (8-1,KO 5),  wote wa hapa nchini.

Alisema vilevile kuwa kesho, Alphonce Mchumiatumbo (9-0, KO 8) atachuana na DeAndre 'Showtime' McCole kutoka Marekani katika pambano la raundi 10 huku Cosmas Cheka (8-3) akitwangana na Alan Kamote (20-6, KO 12) raundi sita.

Rais wa WBF, Howard Goldberg, alisema kuwa shirikisho lake limeamua kuyaleta mapambano hayo nchini kwa lengo la kukuza mchezo wa ngumi Tanzania na hiyo imetokana na kutambua vipaji vya mabondia wake.

"Hata kama Cheka atashinda, ni lazima aende Marekani kupambana tena na Phil... na atapanda tena jukwaani kucheza pambano lingine na bondia mwingine wa Marekani," alisema Goldberg.

Akizungumzia pambano hilo, William alisema mpinzani wake asitarajie kupata walau sare kwani yeye amekuja nchini kuendeleza rekodi yake ya kushinda.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA