ZIMBABWE KUPATA UTAWALA MPYA
Raia wa Zimbabwe wanapiga kura
katika uchaguzi wa Urais unaotajwa kuwa na ushindani mkali huku kukiwa
na madai ya udanganyifu. Rais Robert Mugabe wa miaka 89 amesema
atang'atuka ikiwa yeye na chama chake cha Zanu-PF watashindwa.
Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai na chama chake cha Movement for Democratic Change (MDC) wamelalamikia Zanu-PF kwa kuhitilafiana na utaratibu wa uchaguzi ili kunyakua ushindi, lakini chama tawala kimekanusha madai hayo.Shughuli za kampeini zimekua ghasia zozote huku kukiwa na visa vichache sana vya kuwatisha wapiga kura.
Vyama vya Zanu-PF na MDC viliunda serikali ya muungano mwaka wa 2008 baada ya muafaka wa kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi kufuatia matokeo ya Urais yaliyozua utata. Bw.Tsvangirai alishinda awamu ya kwanza, lakini akajiondoa kwa raundi ya pili akilalamikia mashambulizi yaliyolenga wafuasi wake.
Serikali ya Zimbabwe imewapiga marufuku waangalizi wa magharibi kuchunguza uchaguzi wa leo. Hata hivyo Muungano wa Afrika{AU}, Kanda ya Kusini mwa Afrika{SADC} na makundi ya kijamii nchini Zimbabwe yamekubaliwa kufuatilia jinsi uchaguzi utakavyoendeshwa.
Watu milioni 6.4 wamejiandikisha kupiga kura hii, na maelfu walijitokeza kwenye kampeini za uchaguzi. Matokeo yanatarajiwa kutolewa kwa siku tano zijazo.Mwandishi wa BBC aliyeko Harare amesema kuna foleni ndefu katika vituo vya kupigia kura leo ikiwa siku ya mapumzoko kuhakikisha raia wanapata nafasi ya kuamua serikali mpya.
Mshindi wa moja kwa moja sharti apate asili mia 50 ya kura zote kutangazwa Rais. Ikiwa hakuna mgombea atapata kura hizo, raundi ya pili imepangwa kufanyika Septemba 11. Uchaguzi huu ndio wa kwanza kufanyika Zimbabwe chini ya katiba mpya iliyopitishwa mnamo mwezi Machi mwaka huu.