YANGA USO KWA USO NA MTIBWA UWANJA WA TAIFA, J,TANO

MABINGWA wa Ligi Kuu Vodacom Yanga (Pichani) wanatarajiwa kushuka dimbani Jumatano hii kumenyana na Mtibwa Sugar katika mechi ya kirafiki utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.


Kwa upande wa Yanga, itakuwa ni mechi ya pili ya kirafiki tangu warejee kutoka ziara yao Kanda ya Ziwa ambapo katika mechi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, walitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya URA ya Uganda.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga, zinasema mechi hiyo inayotumika kuijenga zaidi timu hiyo, itachezwa kuanzia 10:00 huku wanachama na wapenzi wa timu hiyo wakijionea ubora wa kikosi chao kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu.

“Yanga kwa sasa kumekuwa na usiri mkubwa hata katika mambo ya msingi, na hiyo inatokana na uongozi ulioko madarakani, lakini mimi nakwambia Jumatano tunacheza taifa kwani najua hivyo,” kilisema chanzo hicho.

Mtandao huu ulifanya mpango kumtafuta Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Baraka Kaziguto, ambaye alisema kuwa yawezekana ikawepo japo hawezi kuthibitisha na alipotafutwa Katibu Mkuu, Laurance Mwalusako, alisema atalizungumzia hilo leo.

Naye Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime, alisema yeye taarifa hizo anazo na amejipanga kwa mechi hiyo na kuongeza kuwa hana shaka dhidi ya Yanga kwani ni timu ya kawaida kama nyinginezo.

“Mimi nautambua huo mchezo tunacheza Jumatano na kama ikishindikana tutacheza Jumamosi ila mchezo hupo na mimi nimejipanga ipasavyo,” alisema Mexime.

Aidha, Mexime aliwashangaa viongozi ambao wanalalamikia ratiba ya Ligi Kuu, na kusema kuwa, hata kama mtu ukilalamika kupangwa na timu fulani lazima utacheza nayo tu na kuwataka kuacha imani hizo kwani kila timu lazima icheze.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA