TPBO, PST WALUMBANA KUMGOMBEA CHEKA, MWENYEWE AFURAHIA
Kitendo cha bondia Francis ‘SMG’ Cheka (Pichani) kusaini mkataba wa kupigana na mmalawi, Chiotcha Chimwemwe kimeibua ‘bifu’ baina ya viongozi wawili wa vyama vya ngumi za kulipwa Tanzania vya TPBO Limited na PST.
TPBO na PST zimeingia kwenye mgogoro huo kufuatia
PST kutoa kibali kwa Cheka cha kupigana na Chimwemwe, wakati ikijua TPBO
pia imetoa kibali kwa bondia huyo kupigana mwezi huo na Mmarekani.
Rais wa TPBO, Yassin Abdallah alimtuhumu mwenzake
wa PST, Emmanuel Mlundwa kwa kumpa kibali Cheka kupigana na Chimwemwe
Agosti 10, wakati akiwa amesaini kucheza na Derrick Findley wa Marekani
siku 20 baadaye.
Malumbano hayo yalianza baada ya Abdallah kumtaja
Mlundwa kama kiongozi wa masilahi ambaye anawatumia mabondia kama
matrekta yake ili kujiingizia kipato huku akitolea mifano mapambano
kadhaa yaliyowahi kusimamiwa na PST.
Wakati Mlundwa akimjibu Abdallah kwa kumwambia
kuwa anataka kujidai anajua ngumi wakati hata gloves hajawahi kuvaa na
kufananisha maneno yake na ujinga.
Vyama vya ngumi za kulipwa nchini vimekuwa kwenye
migogoro ya mara kwa mara ya utoaji vibali vya mapambano ya mabondia,
ambapo PST iliwahi kuingia kwenye mgogoro na TPBC kufuatia TPBC kutoa
kibali kwa Karama Nyilawila kupigana na Cheka wakati akitakiwa kutetea
ubingwa wake wa dunia.
Hata hivyo Cheka ambaye sasa yuko kambini jijini
Nairobi, Kenya amebainisha kuwa anaweza kucheza mapambano yote mawili
kwa mwezi Agosti.