STARS TAYARI KUVAANA NA UGANDA, KAPOMBE AITUMIA SALAMU

SAA chache kabla haijashuka dimbani, Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa, kumenyana na wenyeji Uganda, timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars (Pichani) imetumiwa salamu za heri na beki wake, Shomary Kapombe aliye Uholanzi kwenye majaribio.

Kapombe ametuma salamu hizo kupitia ukurasa wake wa Faceboo, akisema; “Go Taifa Stars, go Bocco, go Ngassa, go Chanongo, go Msuva, go Kiemba...,”.
Ujumbe huu pamoja na kuitakia heri Stars katika mchezo wa jioni hii kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, pia unawahamasisha baadhi ya wachezaji aliowataja.
Kapombe anawataka John Bocco ‘Adebayor’, Mrisho Ngassa, Haroun Chanongo, Simon Msuva na Amri Kiemba na wenzao wajitume kubeba jahazi la Stars ifuzu CHAN mwakani Afrika Kusini.
Kapombe alikuwepo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki mbili zilizopita wakati Stars inafungwa 1-0 na Uganda katika mchezo wa kwanza na baada ya hapo, akaenda Uholanzi kwenye majaribio.
Mchezaji mwingine anayekosekana leo, aliyecheza mechi ya kwanza ni Mwinyi Kazimoto aliyetorokea Qatar.
Kikosi cha Stars kinachotarajiwa kuanza jioni hii ni; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David Luhende, Aggrey Morris, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor’, Amri Kiemba na Mrisho Ngassa.
Katika benchi watakuwepo Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Luizio, Mudathir Yahya, Nadir Cannavaro, Haroun Chanongo, Simon Msuva na Vincent Barnabas.
Tayari Stars imekwishaingia Uwanja wa Mandela, kiasi cha saa moja iliyopita na muda si mrefu itaingia uwanjani kuamsha misuli. Mungu ibariki Stars, ibariki Tanzania. Amin.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA