SIMBA YATANGAZA MAUZO YA MWINYI KAZIMOTO

Klabu ya soka ya Simba ya jijini Dar es Salaam imesema kuwa thamani ya kiungo wake nyota, Mwinyi Kazimoto (Pichani), ambaye hivi karibuni alidaiwa kutoroka na kwenda Qatar kufanya majaribio katika klabu ya Lekwhiya inayoshiriki ligi kuu ya nchi hiyo ni dola za Marekani 100,000 (Sh. milioni 160).


Kauli hiyo ya Simba imekuja kufuatia madai kwamba uongozi wa Lekhwiya umeridhishwa na kiwango cha nyota huyo na kuonyesha dalili za kutaka kumsajili.

Kazimoto ambaye tayari amesharejea nchini lakini hajajiunga na kikosi cha Simba kinachojiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, anadaiwa alitoroka nchini akiwa kwenye kambi ya timu ya taifa (Taifa Stars) muda mfupi kabla ya kuelekea Mwanza kuweka kambi ya kujiandaa kwa mechi yao ya wiki iliyopita waliyochapwa ugenini 3-1 dhidi ya Uganda (The Cranes) katika kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani.

Mmoja wa viongozi wa juu wa Simba alisema kuwa baada ya kuelezwa kwa 'mdomo' kwamba klabu hiyo haiko tayari kumsajili Kazimoto kwa dau kubwa, waliwasiliana na kiungo huyo na ndipo alipoamrishwa kurejea nchini.

"Ila walikubali kumlipa mshahara wa dola za Marekani 3,000 (Sh. milioni 4.8), jambo ambalo si baya kama mwenyewe aliridhia... lakini kwa hadhi yake hicho ni kiasi kidogo sana. Wakati tunamsajili kutoka JKT Ruvu tulitumia zaidi ya Sh. milioni 35, lakini sasa thamani yake imepanda," alieleza kiongozi huyo.

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alisema kwamba hajapokea barua rasmi kutoka timu yoyote ndani au nje ya nchi ikieleza nia ya kutaka kumsajili kiungo huyo.

Mtawala alisema kwamba mbali na kuharibu programu za kikosi cha Stars, pia kutokuwapo kwa Kazimoto kambini kutamvuruga kocha Abdallah Kibaden 'King' ambaye alipaswa kuwa na kikosi kamili wakati huu ili kujiandaa na Ligi Kuu ya Bara.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA