SIMBA YAINGIZWA MKENGE, YATOSA NYOTA WAKE WOTE WA KIGENI
Uongozi wa klabu ya Simba umewatosa jumla wachezaji wote wa kigeni waliokuwa wakijaribiwa kwa matumaini ya kuwamo katika kikosi chao cha Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu ujao (2013/2014) huku pia ikisitisha mkataba wa Mganda Musa Mude aliyeichezea timu yao msimu uliopita, imeelezwa jana.
Mude aliingia mkataba wa miaka miwili na Simba mwaka jana na hivyo kabla ya kusitishiwa mkataba wake, alibakiza mwaka mwingine mmoja kuichezea klabu hiyo ya 'Wekundu wa Msimbazi'.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alisema tayari mchezaji huyo ameshalipwa haki zake zote na pia kukabidhiwa tiketi ya ndege ya kurejea nyumbani kwao Uganda juzi.
Mude ambaye alikuwamo katika kikosi cha Simba kilichomaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa mwisho wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita, hakupatikana jana kuzungumzia kuachwa kwake na pia hatma yake baada ya kuondoka Msimbazi.
Katika hatua nyingine, Mtawala alisema vilevile kuwa klabu hiyo imeachana na mpango wowote wa kutaka kuwasajili wachezaji wengine wa kigeni waliokuwa wakiwafanyia majaribio ambao ni pamoja na Waganda Samuel Ssenkoomi na Assumani Buyinza, Felix Cuipo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na James Kun kutoka Sudan Kusini.
Katibu huyo aliongeza kuwa maamuzi ya kuwaacha Mudde na kina Ssenkoomi yamefanywa na kamati yao ya usajili iliyo chini ya mwenyekiti wake, Zacharia Hanspoppe; ikiwa ni baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa benchi la ufundi kwamba wachezaji hao hawajaonyesha viwango vya juu kwa namna ilivyotarajiwa.
Kutokana na maamuzi hayo mazito ya uongozi wa Simba, sasa kikosi chao kimebakiwa na wageni wawili tu ambao ni kipa wa kimataifa wa Uganda, Abel Dhaira na Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Burundi msimu uliopita, Mrundi Amissi Tambwe aliyesajiliwa kutoka Vital'O ya Burundi.
Habari zaidi kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kwamba uongozi wa klabu hiyo umeanza mazungumzo na beki wa Uganda, Joseph Owino ambaye aliwahi kuichezea Simba na sasa akiitumikia klabu ya URA inayoshiriki Ligi Kuu ya Uganda.
Owino ambaye pia aliwahi kuichezea klabu ya Azam anadaiwa kutaja dau kubwa na sasa viongozi wa 'Wanamsimbazi' wanaendelea kuzungumza naye ili wafikie makubaliano na mwishowe kumsajili baada ya kuvutiwa na kiwango cha juu alichoonyesha wakati URA ilipocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Taifa wiki iliuopita na kuwaadhiri wenyeji kwa kuwachapa 2-1.
Pia klabu hiyo inadaiwa iko katika mazungumzo kwa nia ya kumsajili Mganda Moses Oloya anayecheza soka la kulipwa nchini Vietnam ili ajiunge na Simba katika kipindi cha usajili wa dirisha la Novemba, 2013.