RAGE AFUTA NDOTO YA SIMBA KUMILIKI UWANJA WAKE, KAULI YAKE YAZUA UTATA CCM

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage (Pichani) ameifuta ndoto ya klabu hiyo kuwa na uwanja wake, baada ya kusema haiwezekani uongozi wake kujenga uwanja katika miaka miwili wakati Serikali imejenga Uwanja wa Taifa kwa miaka 50.
Rage alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki kwenye mkutano mkuu wa klabu hiyo uliofanyika Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay huku ukitawaliwa na vurugu zilizosababisha ajenda za muhimu za mkutano kushindwa kujadiliwa kwa kina.
‘’ Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi CCM imewachukua miaka 50 kujenga uwanja wa kisasa ule wa Taifa, sasa mimi Rage na Kamati yangu tutajenga uwanja wa kisasa kwa miaka miwili uwezo huo tunatolea wapi? “alihoji “Vitu vingine vinahitaji kufikiria kwa kawaida tu jamani. Tunaomba muwe wavumilivu tunaenda polepole, lakini kwa uhakika tumeshalipia eneo la ujenzi tunasubiri hati yetu.
Kauli hiyo ilizua majadiliano kutoka kwa wajumbe, lakini Rage aliendelea kusema  ‘’nipo kwenye agenda ya saba nyie pigeni kelele tu mimi naendelea (huku akicheka).
Hapa kuna watu wanataka kwenda kuangalia mpira, tena mtaingia bure na  vitambulisho vyenu, vya mkutano, Simba oyeeee’’.
Licha ya Rage kutoa kauli hiyo, mwenyekiti huyo amekuwa akitoa kauli tofauti tangu alipoingia madarakani juu ya ujenzi wa uwanja huo ambao umebaki kuwa ni ndoto.
Baadhi ya kauli zake ambazo amewahi kuzitoa ni hizi, Desemba 17/2010, alisema mradi wa kujenga uwanja huko Bunju kwa ajili ya timu yao unaendelea vizuri, lakini  mwekezaji wao kutoka Uturuki ambaye alitarajia kuja hivi karibuni atawasili mwakani mara baada ya kupita Sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya.
 “Kwa sasa tumebuni mradi ambao utasaidia kupata fedha kama sh 100 milioni ambazo zinatakiwa kulipia uwanja wetu.
 Mradi huo ni uuzwaji wa jezi ambazo zitauzwa kati ya sh10,000 na 15,000 kwa wanachama wa Simba kwa ajili ya kuchangia gharama za kulipia kitalu hicho.
Novemba 29/2010, Rage alitangaza mipango ya kujenga uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000, eneo la Bunju na ujenzi utasimamiwa na Kampuni ya Uturuki GIDS, na akajikamba ni mabingwa wa ujenzi wa viwanja.
“Uwanja utazungukwa na maduka ya kisasa (Mall) na aliunda timu akiwemo aliyekuwa Makamu Mwenyekiti aliyebwaga manyanga Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Francis Waya, Katibu Mkuu wao Evodius Mtawala.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA