MASIKINI, YANGA KIMENUKA, KIONGOZI WAO AACHIA NGAZI....
Mkurugenzi wa Fedha wa Klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Denis
Oundo amejiuzulu nafasi hiyo miezi 10 tangu alipoajiriwa kuongoza Idara
ya Fedha Jangwani.
Habari za ndani ambazo tumezipata,
zinasema kuwa Oundo ameandika barua ya kuacha kazi akipinga mwenendo
mbovu wa uongozi ndani ya klabu hiyo.
“Amechoshwa kufanya kazi kwa kushinikizwa. Mfano,
pesa za zawadi za Vodacom na udhamini kutoka TBL, ameshinikizwa
aziingize kwenye akaunti binafsi ya kiongozi mmoja wa juu wa klabu
hiyo,” alisema mtoa habari.
Inadaiwa kuwa kiongozi huyo anataka pesa hizo ziingie kwenye akaunti yake binafsi kwa sababu anaidai klabu.
Oundo alikuwa akiwalipa baadhi ya wachezaji fedha
zao za usajili kwa vile walisajiliwa kwa mali kauli, lakini kuna
kiongozi mmoja anashinikiza aanze kulipwa yeye kwanza pesa zake.
Chanzo hicho kilisema pia kuwa, hata fedha za
ubingwa Sh100 milioni walizoahidiwa wachezaji na uongozi, zimeota mbawa
kwani hakuna mpango wowote kwa sasa.
Alipoulizwa Katibu Mkuu wa Yanga, Laurance
Mwalusako kuhusu suala hilo, alishtuka na kuhoji mwandishi amezipata
wapi taarifa hizo.
“Nani kakupa taarifa hizi? Mimi sijui na wala sina barua yoyote ya kujiuzulu kiongozi,” alisema Mwalusako.
Gazeti hili lilimtafuta Oundo aliyesema: “Kama
kuna taarifa zozote kuhusu mimi kuandika barua ya kujiuzulu, basi
zitatolewa kwa utaratibu maalum wa klabu.” Taarifa zaidi zilidai kuwa
uongozi umepokea barua ya kujiuzulu kwa mkurugenzi huyo na umebariki.