LADY JAYDEE KUVAMIA JIJI LA ARUSHA, KULA IDD NA MASHABIKI WAKE

Nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Judith Wambura (Pichani)  anatarajia kuadhimisha miaka 13 ya uwapo wake kwenye tasnia ya muziki jijini Arusha siku ya Eid Mosi na Eid Pili.

Akizungumza  kwa njia ya simu jana, meneja wa mwanamuziki huyo, Gadna G. Habash alisema, mwanamuziki huyo atafanya maadhimisho hayo akishirikiana na rapa Profesa Jay, ambaye pia ni mwanamuziki wa muda mrefu wa kizazi kipya nchini.

Habash alisema kuwa Jaydee atafanya onyesho la kwanza siku ya Eid Mosi kwenye ukumbi wa “Triple A” na onyesho lake la pili atalifanya kwenye ukumbi wa Botaniko Garden.

Meneja huyo aliongeza kuwa onyesho la Eid Pili litakuwa mahususi kwa ajili ya watoto na litafanyika mchana kuanzia saa 6 hadi saa 12 jioni ambapo watoto watapata fursa ya kuonyesha vipaji vyao kama kuimba, kudansi na kadhalika.

“Unajua Jaydee ni mtu anayekubalika na watu wa rika zote kwa hiyo ameona ni vyema akifanya onyesho hilo mchana ili watoto nao wapate kuburudika pamoja nae na kuonyesha vipaji vyao mbalimbali,” alisema.

Habash aliongeza kuwa kwa sasa Jaydee yuko kambini pamoja na Machozi Band wakijiandaa kwa ajili ya maadhimisho hayo makubwa ambapo mwanadada huyo atatumbuiza “live” kwa kutumia bendi yake hiyo.

Maadhimisho hayo ya miaka 13 ya Jaydee yatakuwa ni ya pili kufanyika baada ya yale yaliyoyafanywa mwezi Juni Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya mashabiki waliofurika kwenye ukumbi wake wa Nyumbani Lounge na sasa anatarajia kuzunguka kwenye mikoa zaidi ili kuwafikia wapenzi wake wengi.

Jaydee ni kati ya wanamuziki wa kike waliodumu kwenye sanaa ya muziki bila kutetereka kwa miaka 13 na ametoa jumla ya albamu sita ambazo ni Machozi (2000), Binti (2003), Moto (2005), Shukrani (2007), The Best of Lady Jaydee (2012) na inayotamba sasa ya 'Nothing but the Truth' yenye wimbo 'Joto Hasira'.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA