KOCHA YANGA AWACHIMBA MKWARA NYOTA WAPYA
Benchi la ufundi la Yanga limewataka wachezaji wapya
wa timu hiyo kuonysha uwezo wao mazoezini ili kumshawishi kocha kuwapa
nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo badala ya
kutegemea mtelemko kwenye kupata namba kwa sababu tu ni wapya.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Fred Felix
'Minziro' (Pichani) alisema timu imefanya usajili wa wachezaji wapya lakini
wachezaji hao hawajahakikishiwa namba ya kwenye kikosi cha kwanza cha
timu hiyo.
"Ukiangalia ushindani mkubwa upo kwenye safu ya ushambuliaji kwa sababu Javu (Hussein) ameongezeka," alisema Minziro.
"Lakini hii ni changamoto kwa wachezaji
wote wapya na hata wale waliokuwepo msimu uliopita kuhakikisha
wanajituma ili kupata nafasi."
Alisema makocha hawataangalia jina la mchezaji bali uwezo wake ambao ndiyo utakaompa namba kwenye kikosi cha kwanza.
Alisema kila mchezaji ana nafasi sawa ya
kucheza isipokuwa juhudi na kujituma kwake ndiyo "tiketi" yake ya kupata
namba kwenye kikosi cha kwanza.
Kusajaliwa kwa Javu kunafanya kikosi cha Yanga kuwa na wachezaji sita wa nafasi ya ushambuliaji.
Wachezaji hao mbali na Javu ni Said
Bahanuzi, Jerry Tegete, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngasa ambaye hata hivyo
kocha Ernest Brandts anaweza akamtumia kama winga na Hamis Kiiza ambaye
inasemekana Yanga imeamua kumuongeza mkataba hatimaye.
Yanga itafungua pazia la ligi kuu ya Bara
msimu ujao kwa kucheza na Ashanti United Agosti 24 kwenye Uwanja wa
Taifa lakini wiki moja kabla ya mechi hiyo itacheza na Azam kwenye
mchezo wa Ngao ya Hisani.