KLABU LIGI KUU ZAPONDA RATIBA, ZADAI AZAM IMEBEBWA
Mkurugenzi wa Coastal Union, Nassor Binslum
Mojawapo ya timu zinazolalamikia ligi hiyo ni Coastal Union ya Tanga iliyowahi kutwaa ubingwa wa Bara mwaka 1988, ikida kwamba ratiba ya msimu ujao unaoanza Agosti 24 'inawaumiza' wao na kuwabeba baadhi ya mahasimu wao.
Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Coastal Union, Nassor Binslum, alisema kuwa anashangaa kuona kuwa katika msimu wa tatu mfululizo tangu warejee katika ligi hiyo wakiendelea kupangiwa ratiba inayoonyesha kuwa wanaanzia nyumbani kwao kwenye Uwanja wa Mkwakwani kuzikabili Simba na Mtibwa Sugar katika mzunguko wa kwanza na kumalizia ugenini na wapinzani hao hao.
Binslum alisema kuwa ratiba hiyo pia inaonyesha baadhi ya timu kama mabingwa watetezi, Yanga, wakicheza mechi zao zote mbili jijini Mbeya dhidi ya Prisons na Mbeya City wakati wao (Coastal) wakilazimika kusafiri mara mbili kwenda Mbeya kuzikabili timu hizo.
"Nashangazwa na upangaji huu. Sisi tunakwenda Mbeya kucheza na Mbeya City mzunguko wa kwanza halafu raundi ya pili pia tufunge safari ya kucheza na Prisons... sasa sijui kama ni sawa katika taratibu za kupanga ratiba au vipi," alihoji kiongozi huyo.
Kiongozi mmoja wa JKT Ruvu alikaririwa juzi kupitia luninga akilalamika kuwa ratiba hiyo imewaumiza wao katika baadhi ya mechi kwa kuwapangia katika siku zilizokaribiana sana na hivyo kuwapa muda mfupi tu wa kupumzika.
Kocha wa Ruvu Shooting, Boniface Mkwasa, alisema kuwa baadhi ya mechi zao kwenye ratiba hiyo zinaonyesha kuwa ni kama imekopiwa ya miaka iliyopita, lakini kwa ujumla haoni kama ina tatizo kubwa kama itafuatwa.
"Mechi yetu dhidi ya Prisons imekaa vile vile kama ilivyokuwa msimu uliopita... ila tunaona (ratiba) imezingatia muda wa timu kusafiri kwa kuondoa mechi za Jumatatu," alisema kocha huyo.
Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Saad Kawemba, aliwataka viongozi wa timu zote ambazo zinahisi kuumizwa kutokana na ratiba hiyo kuwasilisha hoja zao kwa maandishi mapema ili zifanyiwe kazi na kuondoa kasoro zitakazobainika kabla ya ligi hiyo kuanza.
Kawemba alisema kwamba watakapogundua kuwa kweli kuna matatizo ya msingi katika ratiba hiyo, kamwe hawatasita kuirekebisha.
"Ni kweli kwamba baadhi ya timu zinaonekana zikicheza mechi nyingi Dar es Salaam na nyingine za ugenini ... hii inatokana na ukweli kuwa Dar ina timu sita na kamati yake ilitaka timu itakayoanzia kwenda Kagera kucheza dhidi ya Kagera Sugar basi iende pia Tabora kumalizana na Rhino Rangers... lakini miundombinu pia ni kikwazo kikubwa na imefikiriwa wakati wa upangaji ratiba," alieleza Kawemba.
Ligi hiyo itakayomalizika April 27, 2014 ndiyo ya juu kwa ngazi ya klabu Tanzania Bara na pia ndiyo inayotoa wawakilishi wa Bara katika michuano ya klabu ya kimataifa ikiwamo ya ligi ya klabu bingwa na Kombe la Shirikisho.