SIMBA BADO HAIJAPATA BEKI WA KATI-KIBADEN

Kocha wa klabu ya Simba, Abdallah Kibadeni (Pichani), amesema kikosi chake kipo tayari kwa ligi kuu ya Bara lakini bado anahitaji beki wa kati mwenye uwezo mkubwa.


Akizungumza  kwa njia ya simu kutoka kambini Kigamboni jiji la Dar es Salaam, Kibadeni alisema amepata kikosi chake cha kwanza lakini anataka kuongeza nguvu kwenye safu ya ulinzi ya timu hiyo.

"Tumefanya mazoezi kwa muda mrefu sasa na tayari nimewafahamu wachezaji wangu na uwezo wao," alisema Kibadeni ambaye ni kocha bora wa mwaka jana kwa kuiwezesha Kagera Sugar kushika nafasi ya nne licha ya udogo wa timu.

"Kwangu timu imekamilika na vitu vilivyobakia ni kidogo sana... naangalia sana safu yangu ya ulinzi."

Alisema ameshatoa maombi kwa uongozi wa timu hiyo ili kutafutiwa beki wa kati na kwamba viongozi hao wapo kwenye mazungumzo na baadhi ya wachezaji wa nje ya nchi kwa ajili ya kuona uwezekano wa kuwasajili.

Mmoja wa mabeki wa kati ambao Simba kwa sasa ipo kwenye mazungumzo nao ni mchezaji wake wa zamani, Joseph Owino wa URA ya Uganda.

Owino aliwahi kuichezea kwa mafanikio Simba miaka miwili iliyopita kabla ya kuachwa na kwenda Azam msimu mmoja, na kurudi Uganda kujiunga na URA.

Kibadeni alisema anataka Simba isajili beki mwenye uwezo na uzoefu ili kuisaidia timu kwenye ligi kuu inayatorajiwa kuanza Agosti 24.

Alipoulizwa juu ya Owino, Kibadeni alisema uongozi wa klabu hiyo unamfuatilia mchezaji huyo na kusema endapo atasajiliwa kwenye timu hiyo atakuwa msaada mkubwa katika harakati za kutaka kutwaa ubingwa msimu huu.

Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hanspope alikaririwa na vyombo vya habari akisema wanafanya mazungumzo na Owino kwa lengo la kumsajili baada ya kuwasiliana na Kibadeni.

Wakati Simba wakitafuta beki wa kati, kikosi hicho pia kipo hatarini kumpoteza beki wake kiraka, Shomari Kapombe ambaye amekwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini Uholanzi.

Endapo Kapombe atafanikiwa na kupata timu nchini humo, Simba itawalazimu kutafuta mbadala wake.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA