KIBADEN AIHOFIA RHINO RANGERS, ADAI ITAWAKAMIA
Akizungumza jana, Kibadeni
alisema katika kuhakikisha timu yake inakuwa tayari kwa ajili ya mchezo
huo dhidi ya Rhino, Simba itacheza mechi nne zaidi za kirafiki ikiwemo
ya leo dhidi ya Coastal Union, mjini Tanga.
Simba itacheza na Rhino Rangers kwenye
uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mjini Tabora Agosti 24 na Kibadeni amesema
kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kwa kuwa Rhino Rangers watataka kuonyesha
umwamba wake baada ya kupanda daraja.
Alisema kuwa kwa kuanzia Simba leo
wanashuka kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga kucheza na Coastal
Union kwenye mchezo wa kirafiki.
Kocha huyo wa Simba amesema mchezo huo ni kati ya mchezo minne ya kirafiki aliyopanga kucheza kabla ya kuanza kwa ligi kuu.
"Kupangwa kuanza na timu ngeni kwenye ligi
mara nyingi mchezo unakuwa mgumu kwa sababu naamini Rhino Rangers
watatukamia," alisema Kibadeni.
Kibadeni amerudi kufundisha Simba baada ya
kuwa kocha bora wa mwaka jana alipoiwezesha Kagera Sugar kushika nafasi
ya nne kwenye ligi kuu ya Bara licha ya udogo wa timu hiyo ya Bukoba.
"Tunaendelea na maandalizi michezo (na)
minne au mitatu ya kirafiki itatuweka vizuri kuwakabili Rhino kwenye
ligi," alisema Kibadeni.
Alisema kuwa baada ya mchezo huo wa leo
dhidi ya Coastal Union, Simba itacheza micheo mingine miwili kabla ya
kucheza mchezo wa mwisho wa kirafiki kwenye kilele cha Siku ya Simba
'Simba Day' Agosti 8 mwaka huu.
Akizungumzia kikosi chake, Kibadeni
alisema tayari amepata timu ya kwanza na kwa sasa anakazania mfumo
atakaokuwa akiutumia kwenye ligi.
"Kikosi changu kipo tayari na mimi kama kocha najua kikosi changu cha kwanza," alisema Kibadeni na kueleza zaidi:
"Kwa sasa kikubwa ninachokifanya ni kuwazoesha mfumo ninaotaka kuutumia kwenye ligi na mashindano mengine."
Alisema hatakuwa na mfumo mmoja, hata
hivyo, bali ameandaa mifumo mitatu atakayokuwa akiitumia kulingana na
mbinu za timu wanayocheza nayo.
Mchezo dhidi ya Coastal Union utakuwa wa
kwanza wa Simba tangu kupata kipigo cha magoli 2-1 kutoka kwa URA ya
Uganda kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja
wa Taifa wiki mbili zilizopita.