KASEJA ATOBOA SIRI YA KIPIGO CHA JANA
NAHODHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Juma Kaseja (Pichani akiangalia mpira ukitinga kimiani) amewataka mashabiki wa soka nchini kubadilisha mitazamo yao kwamba wachezaji chupikizi ndiyo wanaofaa kuliko wakongwe.Akizungumza jana mjini hapa, Kaseja alisema kwamba mashabiki wamekuwa wakitaka sana wachezaji chipukizi wapewe nafasi, lakini ukweli ni kwamba hawamudu kabisa.
“Tusaidieni kuwaelimisha mashabiki, wao wanataka sana wachezaji chipukizi, lakini nadhani mmeona leo, hawawezi. Wanahitaji kupewa muda wakomae taratibu. Hata sisi tulipokuwa chipukizi, tulikomazwa taratibu,”alisema Kaseja.
Ingawa Kaseja hakuweka wazi, lakini inaonekana alikuwa anawazungumzia wachezaji chipukizi walivyoigharimu Stars jana ikitolewa na Uganda katika michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, ikafungwa na Uganda mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa.
Beki chipukizi, David Luhende aliyeitwa Stars kwa mara ya kwanza safari hii, aliunawa mpira akiwa peke yake- baada ya kushindwa kuumilii vyema na kusababisha penalti, wakati huo timu hizo zikiwa zimefungana 1-1 na Brian Majwega akaifungia Uganda bao la pili.
Kiungo chipukizi, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliyepandishwa timu hiyo Mei mwaka jana, alijaribu kuwapiga chenga wachezaji wawili wa Uganda, wakati huo wachezaji karibu wote wa Tanzania wamepanda kufuata shambulizi la kona, akapokonywa mpira na likafanywa shambulizi la kushitukiza, Stars ikafungwa bao la tatu.
Wachezaji wengine chipukizi walioingizwa kipindi cha pili, Simon Msuva na Haroun Chanongo walishindwa kuisaidia timu kubadilisha matokeo japo kidogo.