HUMUD SAFI SIMBA, KULAMBA MAMILIONI KUICHEZEA MSIMU UJAO

Kiungo mkabaji wa zamani Azam FC, Abdulhalim Humoud (Pichani) ameibukia Simba akisaka nafasi ya kusajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Humoud aliyemaliza mkataba wake na Azam FC Mei, mwaka huu na kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa na klabu ya Jomo Cosmos, yuko kambi ya Simba iliyopo, Kigamboni, Dar es Salaam.
Akizungumza jana, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are alithibitisha mchezaji huyo kuwepo kwenye kambi ya timu yake akisaka nafasi kwa ajili ya msimu ujao wa ligi,  Agosti 24.
Itang’are alisema kuwa Kocha Abdallah Kibadeni ndiye aliyemtaka mchezaji huyo anayedaiwa kufuzu na klabu ya Jomo Cosmos.
“Kocha ndiye ametaka aje kambini kufanya mazoezi na timu ili aweze kujiridhisha na kiwango chake kabla ya kusaini mkataba,” alisema na kuongeza.
“Kamati ya Usajili Simba, tunasubiri kauli ya mwisho kutoka benchi la ufundi na kufanya naye makubaliano ya kusaini mkataba.”
Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema jana kuwa, yuko kwenye kambi ya Simba kwa siku tano sasa akifanya mazoezi na wachezaji wenzake.
“Maendeleo yake ni mazuri ingawa siwezi kusema lolote kwa sasa. Ni mchezaji ambaye namjua vizuri, siyo mgeni kwangu. Pia najua aliwahi kuichezea Simba kipindi cha nyuma kabla ya Azam FC.” alisema Kibadeni.
Humoud alipofuatwa na gazeti hili baada ya kumaliza mazoezi alisema: “Sitaki kuzungumza lolote kwa sasa, ni mapema.”
Humoud alijiunga na Simba akitokea Mtibwa Sugar na kutolewa kwa mkopo na klabu hiyo kwenda Azam FC.
Wakati huohuo, mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Hussein Javu amejiunga na mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga na jana asubuhi alifanya mazoezi.
Javu aliyekuwa akitolewa macho na Simba, amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili mpaka mwaka 2015.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA