BREKING NEWS: HAMISI KIIZA HUYOOOO COASTAL UNION.......
Coastal Union ya Tanga, imeendelea na dhamira yake ya
kuvibomoa vigogo vya soka nchini, baada ya juzi kupiga hodi Yanga
wakitaka kumsajili mshambuliaji asiyetulia Jangwani, Mganda Hamis Kiiza (Pichani).
Union imekuwa ikifuatilia kwa karibu mzozo wa
kimasilahi kati ya Kiiza na uongozi wa Yanga, kabla ya mwanzoni mwa wiki
kufikia uamuzi wa kuweka mezani Dola 25,000 ili kumchomoa nyota huyo.
Kama hatua hiyo itafanikiwa, basi Kiiza ataungana
na wachezaji wengine watatu waliosajiliwa na Coastal, Haruna Moshi
‘Boban’, Juma Nyoso kutoka Simba na Uhuru Seleman aliyekuwa akicheza kwa
mkopo Azam FC.
Kiiza, aliyekuwa kiini cha mafanikio Jangwani
msimu uliopita hata kuiwezesha klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Bara,
hajasaini mkataba mpya kwa kile kilichoelezwa kutaka dau kubwa kuliko
uwezo wa Yanga.
Akizungumza jana, kiongozi mmoja wa
Coastal Union ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini kwa kuwa
siyo msemaji, alikiri kuwepo mpango huo.
“Ni kweli, tumepeleka ofa Jangwani kutaka
kumsajili Kiiza, na kinachoendelea sasa ni kufanya mazungumzo na
mchezaji huyo ili tujue hatima ya baadaye,” alisema kiongozi huyo.
“Tunajua Kiiza ni mchezaji mzuri, na dau lake
lazima liwe nzuri. Hatuna shaka na uwezo wake, tuko tayari kutoa dola
25,000 (Sh39.5 milioni) ili aje kucheza Uwanja wa Mkwakwani,” aliongeza.
Mapema wiki iliyopita Mwenyekiti wa Kamati ya
Usajili Yanga Abdallah Binkleb, alikaririwa akisema kutokuwapo uwezekano
wowote wa klabu hiyo kumpiga bei Kiiza.
“Tunamuhitaji Kiiza, ni mchezaji mzuri na bado
mchango wake unatakiwa. Hatuwezi na wala hatuna mpango wa kumuuza kwa
sasa pamoja na kutaka dau kubwa ili abaki,” alisema Binkleb.
Kiiza amegoma kusajili Yanga akitaka kulipwa Dola
40,000 (Sh63.2 milioni). Lakini uongozi wa Yanga umemtaka kuchukua Dola
35,000 (Sh55 milioni) na kiasi cha Dola 5,000 (Sh7.9 milioni) anunuliwe
gari, uamuzi aliopinga mchezaji huyo.
Klabu ya nchini kwake Uganda, URA nayo ilielezwa
kuwa tayari kutoa Dola 40,000 ambazo Yanga wanashindwa kumpa Kiiza na
mshahara wa mwezi Dola 1,000 ili arudi kucheza Ligi ya Uganda.
Kwa upande wa msemaji wa Coastal, Eddo Kumwembe alithibitisha klabu hiyo kutuma maombi ya kumsajili Kiiza.