Yosso wawili waenda Qatar kunolewa

Angetile Osiah
Wachezaji yosso wawili wa hapa nchini wamechaguliwa kuingia katika kituo cha kuendeleza vipaji kilichoko jijini Doha, Qatar kupitia mpango wa kukuza vipaji wa Aspire Football Drea baada ya kufuzu majaribio nchini Uganda.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Katibu Mkuu wa shirikisho la soka (TFF) Angetile Osiah alisema wachezaji waliochaguliwa kujiunga na kituo hicho ni Abdulrasul Tahir Bitebo (15) ambaye ni mshambuliaji kutoka Kituo cha Uwanja wa Karume, na Martin Omela Tangazi (14) ambaye ni beki kutoka Kituo cha Ukonga.

Bitebo ni mtoto wa mshambuliaji wa zamani wa timu ya Pamba ya Mwanza, Khalid Bitebo.

Osiah alisema yosso hao wawili wanaungana na mchezaji mwingiene mmoja kutoka nchini Kenya na kufanya idadai ya wachezaji watatu wanaotakiwa kujiunga na kituo hicho kutoka Afrika Mashariki.

"Wachezaji wengine walikuwa wakitoka katika nchi za Uganda na Kenya," alisema Osiah na kueleza zaidi:

"Hii ni fahari kwetu kwa sababu vijana waliokuwa wakitakiwa katika kundi hilo la vijana 50 ni watatu na sisi tumetoa wachezaji wawili kati ya watatu."

Osiha alisema taratibu za safari ya wachezaji hao zinaendelea kufanyika na baada ya kukamilika watataja siku ya kuondoka wachezaji hao.
Mpango wa 'Aspire Football Dream' unafadhiliwa na Mtoto wa Mfalme wa Qatar katika nchi 16 duniani, na kwa hapa nchini uko chini ya Idara ya Ufundi ya TFF.

TFF ina jumla ya vituo 14 vya kuendeleza vipaji kupitia mpango huo wa Aspire Football Dream.

Vituo hivyo ni Karume, Kigamboni, Tandika, Kawe, Ukonga, Kitunda, Mbagala, Magomeni, Makongo na Tabata vilivyo katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Vingine ni Bagamoyo kilichopo mkoani Pwani, Morogoro, Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI