Profesa Jay, Jide wang'ara tena tuzo za Kill

Lady Jaydee, ambaye anashikilia tuzo ya mwanamuziki bora wa kike, akipagawisha mashabiki wakati wa uzinduzi wa ziara ya kimuziki ya Kili kwenye uwanja wa Jamhuri Mkoani Dodoma, juzi Jumamosi.
Ziara ya mikoa 10 ya kimuziki yenye lengo la kuupa nguvu muziki wa Kitanzania na utamaduni wake kwa ujumla, ilianza juzi katika viwanja vya Jamhuri mkoani Dodoma na kujumuisha wanamuziki saba wanaong'ara katika tasnia ya muziki Tanzania huku wakongwe na chipukizi wakitoana jasho.
Ziara hiyo iliyodhaminiwa na kampuni ya bia ya TBL kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro, ilijumuisha wanamuziki mchanganyiko kama Judith Wambura, Linex Sunday, Roma Mkatoliki, Ommy Dimpoz, Kala Jeremiah, Profesa Jay na mkali wa muziki wa R&B nchini Ben Pol.
Wanamuziki waliotia fora katika tamasha hilo ambalo wiki ijayo linatarajia kuelekea katika mkoa wa Tanga ni Ben Pol ambaye alikuwa wa pili kupanda jukwaani. Mashabiki walionekana dhahiri kumuelewa na kuitikia kila wimbo aliokuwa akiimba na kusababisha wakati mwingine yeye kukaa kimya na kuachia mashabiki hao waimbe mwanzo hadi mwisho wa wimbo.
 
Ben Pol alipanda na wimbo 'Maneno Maneno' na kusababisha shangwe kubwa uwanjani, na baada ya hapo, aliimba nyimbo zake maarufu kama 'Pete', 'Jikubali', 'Samboira', 'Nikikupata' na 'Maumivu'.
 
Lady Jaydee alikuwa ni mwanamuziki mwingine aliyeshangiliwa sana, baada ya kupanda jukwaani akiwa bila bendi, jukwaa ambalo aliacha kupanda kwa takriban miaka saba sasa, mara baada ya kuanzisha bendi yake ya Machozi.
 
Jaydee alipanda jukwaani na wimbo aliomshirikisha marehemu Albert Mangweha, ambapo baada ya kumaliza alisema ni heshima yake kwa kijana huyo ambaye ameacha alama katika muziki wa kizazi kipya nchini. Baada ya hapo aliendelea na vibao kama 'Wangu', ambapo alikuwa akiimba na kurap mwenyewe, hali iliyosababisha uwanja mzima wa Jamhuri kushangilia muda wote aliokuwa akiimba.
 
Ulipofikia wakati wa kuimba wimbo wa 'Joto Hasira', akasindikizwa na Profesa Jay ambaye alizidi kupagawisha maelfu ya wakazi wa Dodoma waliokuwa wamefurika uwanjani hapo kuangalia uzinduzi wa ziara hiyo ya muziki ya Kili ambayo mwaka huu haijumuishi washindi wa tuzo kama ilivyo kawaida, bali wasanii wanaong'ara katika medani ya muziki wa kizazi kipya.
 
Akiongea baada ya onesho hilo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, ambaye alionekana kufurahia onyesho alifafanua kwamba kampuni yake, kupitia bia ya Kilimanjaro imedhamiria kuupeleka muziki wa Tanzania katika hadhi yake na ndio maana mwaka huu, imebeba mandhari ya kikwetukwetu, ili kuipa sanaa ya Kitanzania nafasi ya kutambulika.
 
Ziara hiyo inatarajia kuendelea wiki ijayo katika mkoa wa Tanga kabla ya kuelekea Moshi wiki inayofuata

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI