YANGA KUANZA KUTETEA KAGAME J,PILI

MABINGWA watetezi wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga wanatarajia kuanza mazoezi Jumapili kwa ajili ya kujianda na michuano hiyo ambayo mwaka huu itafanyika nchini Sudan, Hata hivyo, mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara wataanza mazoezi bila ya nyota wake walioko kwenye kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars).

Akizungumza na MAMBO UWANJANI, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa tayari wameshawapa taarifa ya kuanza kwa mazoezi hayo wachezaji ambao hawako kwenye kikosi cha Taifa Stars na kuongeza kwamba kocha Mholanzi Ernie Brandts, atarejea nchini Jumapili akitokea kwao alikoenda kwa mapumziko.

Saleh alisema kwamba kocha alielekeza kuanza mazoezi siku hiyo akiamini kwamba nyota walioko Stars nao wanaendelea kujinoa na watakaporejea nchini wataimarisha kasi.

Alisema katika ripoti yake amehitaji mechi moja ya kirafiki kabla ya kuelekea Sudan katika mashindano hayo yatakayoshirikisha timu 13 za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

"Ila sijui itakuaje kwa wachezaji ambao mikataba yao imeisha na mpaka sasa hawajui hatma yao, ni ngumu mchezaji kufika mazoezini huku akiwa hana uhakika na ajira yake," alisema meneja huyo.

Katika mashindano ya Kombe la Kagame yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na kufanyika kila mwaka, Yanga imepangwa kundi C na itaanza kampeni za kutetea ubingwa wake kwa kuivaa Express ya Uganda kwenye Uwanja wa Alfasher, Juni 20 saa nane mchana na watashuka tena dimbani Juni 22 mwaka huu kuikabili Ports ya Djibout. Watakamilisha mechi za hatua ya makundi Juni 25 kwa kuvaana na Vital'O kutoka Bujumbura, Burundi.

Wawakilishi wengine wa Bara,  Simba wako katika kundi A na wataanza kwa kuivaa El Mereikh Juni 21 kabla ya Juni 23 kuikabili APR ya Rwanda. Watamaliza dhidi ya Elman ya Somalia, Juni 26.

Mechi ya ufunguzi wa mashindano hayo itakayofanyika Juni 18 saa nane mchana itazikutania Tusker ya Kenya dhidi ya Super Falcon ya Zanzibar na saa 10:00 jioni wenyeji Al Hilal watachuana na Al Nasri.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA