Wachezaji wageni Ligi Kuu kubanwa
Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema litakutana na klabu za Ligi Kuu kuzikumbusha azimio la mwaka jana la mjini Bagamoyo kuhusu wachezaji wa kigeni.
Azimio hilo lilipitisha sheria inayokataza klabu za Ligi Kuu kusajili zaidi ya wachezaji watatu kutoka nje ya nchi.
Pamoja na sababu mbalimbali za kupitisha azimio
hilo, dhamira kuu ilikuwa kuwapa fursa wachezaji wa ndani kuonyesha
vipaji vyao kwenye michuano ya ligi.
Kwa sasa, klabu zinaruhusiwa kusajili siyo zaidi
ya wachezaji watano kufikia msimu uliomalizika, lakini kama azimio hilo
litaungwa mkono na klabu, basi msimu wa 2013/14 utashuhudia wachezaji
wachache wa kigeni.
Klabu za Simba, Yanga na Azam ndizo zinaoongoza
kusajili wachezaji wa kigeni kulinganisha na timu zingine zinazoshiriki
ligi hiyo.
Mtendaji Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alikaririwa
na mtandao wa soka nchini Uganda, akisema mchakato huo unaendelea
kufanyiwa kazi na watakutana na viongozi wa klabu kujadili.
“Ni sheria mpya ya Azimio la Bagamoyo. Ni vyema
sheria zilizowekwa na sisi wenyewe zikaheshimika. Tutakutana na klabu
kujadili azimio hili,” alisema Osiah.
Kabla hata ya kufanyika kwa kikao hicho, klabu
hizo zenye utamaduni wa kusajili wachezaji wa kigeni, zilionyesha
kutoridhika nalo.
Katika msimu uliopita klabu ya Azam ilikuwa na
wachezaji wa kimataifa kutoka Kenya, Joackins Atudo na Humphrey Mieno,
Brian Umony kutoka Uganda na wachezaji wawili kutoka Ivory Coast, Kipre
Tchetche na Michael Bolou.
Kwa upande wa Yanga, Haruna Niyonzima kutoka
Rwanda, Mganda Hamis Kiiza na Didier Kavumbagu wa Burundi na Mbuyu
Twite, huku Simba ikiwa na Abel Dhaira, Musa Mudde, Felix Sunzu na
Komabil Keita.
Pamoja na tahadhari hiyo, klabu hizo zimeendelea
na zoezi la kusajili wachezaji wa kigeni bila kufikiria uwepo wa azimio
la Bagamoyo.