Stars yapaa ikiahidi ushindi

KOCHA wa timu ya Taifa Stars, Kim Poulsen
Wakati timu ya taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) ilitarajiwa kuondoka nchini jana usiku kuelekea Addis Ababa kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan, kocha wa timu hiyo, Kim Poulsen, amesema wanaichukulia mechi yao dhidi ya Morocco itakayofanyika Juni 8 mjini Marrakech kuwa ni zaidi ya fainali.

Stars itaanza kwa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan Jumapili Juni 2 katika kuwaandaa nyota wake kuzoea hali ya hewa ya baridi kama iliyoko Marrakech .

Akizungumza na gazeti hili jana asubuhi, Kim alisema kwamba wanafahamu ushindi wa aina yoyote ndiyo utakaowaweka kwenye nafasi ya kufuzu kucheza fainali zijazo za Kombe la Dunia.

Kim alisema kwamba wamejipanga vizuri kwa ajili ya mechi hiyo ya ugenini na kwamba ushindi wa 3-1 walioupata dhidi ya Morocco katika mechi yao ya awali hapa nyumbani unawaongezea kujiamini wakati wenyeji wao watakuwa katika 'presha' kubwa.

Mdenmark huyo alisema kwamba hakuna kisichowezekana katika mchezo wa soka na mwaka huu vijana wake wamedhamiria kuweka rekodi mpya kwa kufanya vizuri katika mechi hizo.

"Tunakwenda kuwafunga Morocco, hiyo ndiyo falsafa tunayoondoka nayo, tunafikiria fainali za Kombe la Dunia na CHAN (mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani) pia, tunaamini tutafuzu kwa sababu tunauwezo na tunapata ushirikiano wa kila aina kutoka kwa wanaotuzunguka," alisema Kim.

Nahodha wa timu hiyo, Juma Kaseja, alisema kwamba wamejiandaa vizuri na kila mmoja kwenye kikosi hicho ana kiu ya mafanikio.

Kaseja alisema kwamba wamedhamiria kutimiza ndoto za kushiriki fainali hizo kubwa zaidi duniani na vile vile kutangaza vyema jina la Tanzania.

"Inshaallah tutashinda, tunaamini hivyo na tumejiandaa vizuri, ni timu yenye chachu ya ushindi na mafanikio," aliongeza.

Timu hiyo inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro ilitarajiwa kuondoka jana saa 5:00 usiku kwa ndege ya Shirika la ndege la Misri ikiwa na wachezaji 21 ambao wanaongozwa na Kaseja.

Kikosi kilichoondoka kinawahusisha pia Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Haroub Nadir 'Cannavaro', Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva na John Bocco.

Wachezaji wengine ni Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd na Haruni Chanongo huku nyota, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu ambao wako na timu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo watajiunga na kikosi jijini Marrakech, Juni 4 wakitokea Maputo, Msumbiji mara baada ya kuitumikia klabu yao katika mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Liga Muculumana ya huko.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA