SIMBA, YANGA KUIPINGA AZAM
Klabu za Simba na Yanga zinafikiria kuupiga chini mkataba wa
udhamini wa Kampuni ya SSB, ambao ni wamiliki wa timu ya Azam na badala
yake kuukubali ule wa Super Sports.
Katibu Mkuu wa Yanga, Laurance Mwalusako alisema
kuwa pamoja na kwamba hawajauona mkataba wa Super Sports, lakini uzoefu
unaonyesha wanaingiza fedha nyingi zaidi kwenye ligi.
“Sisi tunasikia kuna mazungumzo yanafanywa na
Kamati ya Ligi na TFF na Super Sports. Tunavyojua ligi za Uganda na
Kenya, timu zinapata fedha nyingi. Mfano Uganda ni milioni 300 hawana
shida ya mapato ya mlangoni, mechi ijaze, isijaze wao hawajali kwani
tayari wana uwezo wa kujiendesha wenyewe kutokana na udhamini. “Sisi
tulikataa wasionyeshe mechi bure, ila kama watakuja na ofa nzuri tupo
tayari kupokea na kuachana na Azam kwani ofa yao ni nzuri zaidi.”
alisema Mwalusako.
Hivi karibuni, TFF na Kamati ya Ligi walikutana na
klabu za Ligi Kuu kujadili mkataba wa Azam, ambao wanatarajia kutoa
Sh100 milioni kwa kila klabu msimu ujao kama udhamini ili kuonyesha
mechi za ligi.
Hata hivyo kikao hicho kilizua mvutano mkubwa kwa
klabu za Simba na Yanga kutaka kupewa udhamini mnono zaidi kwa vile
ndiyo timu kubwa za soka na kudai hawawezi kupewa mgowo sawa na klabu
nyingine.
Kuhusu vigogo hao wa soka kukutana na kupanga
mikakati ya kupata mapato zaidi kwenye msimu ujao wa Ligi ikiwa ni
pamoja na kuweka mkakati wa kuziachia mapato timu za mikoani Mwalusako
alisema: “Hilo lipo juu ya uwezo wangu. Ni wenyeviti ndiyo walikaa na
kuamua hilo.”