Mwili wa Ngwair kuwasili kesho
Msanii wa bongofleva Albert Mangwea aliyefariki Jumanne nchini Afrika Kusini
Mwili wa nyota huyo utaagwa Jumapili katika eneo bado halijaamuliwa kati ya viwanja Leaders, Biafra au Posta.
Msemaji wa kamati hiyo, Adam Juma, alisema baada ya mwili huo kuagwa, Jumapili jioni safari ya kwenda Kihonda, Morogoro itaanza kwa ajli ya mazishi yatakayofanyika Juni 3, mwaka huu.
"Tunaelewa namna Watanzania wanavyotambua mchango wa marehemu na jinsi alivyowahudumia kwa kuwaburudisha, hivyo tunawaomba wajitokeze kwa wingi siku hiyo katika kumuaga kijana wetu ambaye alikuwa nyota wetu sote," alisema Juma.
Juma alisema kwa kuwa gharama za kusafirisha mwili huo kutoka Afrika Kusini kuja Tanzania na kupelekwa Morogoro, vyakula, viti, matangazo na malazi ni kubwa hivyo wanaomba Watanzania wote kwa ujumla kutoa michango yao ya hali na mali ili kufanikisha msiba huo.
Akataja namba ya simu ya kaka wa marehemu Kenneth Mangwea 0754 967738 kuwa ndiyo itumike kwa michango hiyo.
Kwa upande wake, Addo November, ambaye ni Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, aliwataka Watanzania kutoamini maneno yanayozushwa na watu na mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusu sababu za kifo cha msanii huyo kwakuwa hadi jana hapakuwa na aliyekuwa akifahamu kilichomuua kwani uchunguzi wa daktari ulikuwa haujakamilika.
''Watu wanazusha maneno mengi kwamba eti kuna mtu kaununua msiba huu na ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ndiyo unaosimamia taratibu zote za kusafirisha mwili wa marehemu.
Hayo yote si ya kweli kama utaratibu huo ungekuwapo sisi tungekuwa wa kwanza kujua lakini hakuna taarifa yoyote tuliyopata kuhusiana na mtu kuununua msiba huu, jambo lililopo ni kwamba wananchi wametoa michango yao kama kawaida,'' alisema November.
Meneja wa msanii huyo, Leo Rubama, ambaye amefanya nae kazi marehemu kwa muda wa miaka miwili iliyopita, alisema ameupokea msiba huo kwa masikitiko makubwa na hakuamini alipopokea taarifa hizo kwani aliona kama watu wanazusha.
"Nilishindwa kuamini kabisa nilipopokea taarifa hizo ukiangalia niliongea naye siku moja kabla ya mauti kumkukuta na akiniambia kuwa kesho yake niende uwanja wa ndege (wa kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam) kumpokea," alisema Rubama.
Mtayarishaji wa muziki katika studio ya Bongo Records, Paul Matthysen a.k.a P-Funk 'Majani', alisema msanii huyo alikuwa ni mtu mwenye upendo na ushirikiano mkubwa na alifanya kazi nyingi katika studio yake na kwamba itakuwa vigumu kwake kumsahau na kuamini kama hatamuona tena.
Shirikisho hilo pia liliwakumbusha Watanzania kumuombea msanii Mgaza Pembe a.k.a 'M to The P' ambaye alikuwa pamoja na Mangwair na amelazwa katika hospitali ya St. Hellen nchini Afrika Kusini.
Hali ya 'M to The P' iliendelea kutengemaa baada ya jana kuhamishwa kutoka katika wodi ya wagonjwa mahututi na kupelekea katika wodi ya wagonjwa wa kawaida.