Mwakalebela aibwaga TAKUKURU

Aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela
Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imetupilia mbali rufaa iliyokatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), dhidi ya hukumu ya kuachiwa huru kwa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela (41), na mkewe Selina, katika kesi ya kushawishi na kutoa rushwa katika mchakato wa kura ya maoni ya nafasi ya ubunge ndani ya CCM.


Uamuzi huo ulitolewa jana mahakamani hapo na Jaji Nkuya na kuondolewa kwa kesi hiyo kunafuatia pingamizi la awali lililowekwa na mawakili wa Mwakalebela, Basil Mkwata na Alex Mgongolwa, waliokuwa wakipinga rufaa iliyokatwa na Takukuru dhidi ya hukumu hiyo.

Upande wa utetezi uliweka pingamizi la awali la kuiomba mahakama kutupilia mbali rufaa hiyo iliyokatwa na Takukuru kwa sababu rufaa hiyo haikuambatanishwa na uamuzi uliotolewa na mahakama ya wilaya ya Iringa.

Akiondoa shauri hilo mahakamani, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Festo Lwila, aliyekuwa anasikiliza shauri hilo alisema mahakama imeridhia pingamizi hilo.

Hakimu Lwila alisema mshtakiwa alishtakiwa kwa kutumia sheria mbili tofauti kwenye hati moja ya mashtaka, suala ambalo ni kinyume cha sheria na kinaweza kumsababisha ashindwe kuandaa utetezi wake ipasavyo.

Pia, hakimu Lwila alisema hapakuwa na sababu ya kuweka sheria mbili tofauti kwenye hati moja na kwamba, usahihi wa hati ya mashtaka unapaswa kuwa makini tangu awali inapoandaliwa.

Katika pingamizi hilo, Mkwata alisema tayari mshtakiwa ameshaadhibiwa baada ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kumwengua kwenye uchaguzi, hivyo kuomba shitaka hilo liondolewe mahakamani.

Mwakalebela alikuwa mshindi wa kwanza wa kura za maoni za CCM za nafasi ya ubunge wa Iringa Mjini mwaka jana, lakini jina lake liliondolewa na nafasi yake kupewa Monica Mbega, ambaye alishindwa na mpinzani wake, Mchungaji Peter Msigwa wa Chadema katika uchaguzi wa ubunge.

Awali, akisoma shtaka hilo Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Imani Mizizi, alidai kuwa Juni 20, mwaka jana, Mwakalebela alidaiwa kutoa hongo ya Sh.100,000 kwa Hamis Luhanga ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkoga, ili awagawie wajumbe 30 wa CCM walioitwa kwenye kikao.

Mizizi alidai kuwa, Mwakalebela anadaiwa kutoa rushwa kinyume cha sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kifungu cha 15(1)(b) kinachokwenda sambamba na sheria ya gharama za uchaguzi namba 6 ya mwaka 2010, kifungu cha 21 (1) (a) na kifungu cha 24(8).
Hata hivyo washitakiwa hao walikana shitaka hilo.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA