KIBADEN NOMA, AANZA KAZI SIMBA
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba na timu ya taifa ya Tanzania, jana asubuhi aliongoza mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Kinesi jijini Dar es Salaam, ambayo yalihudhuriwa na wachezaji 11 wapya, wakiwamo Wacongo wanne.
Kibadeni maarufu kama 'King Mputa' ametua Simba ikiwa ni mara yake ya nne, akitokea Kagera Sugar aliyoinoa msimu uliomalizika wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuisaidia kumaliza katika nafasi ya nne na ya mwisho ya kufuzu kucheza michuano midogo ya Ligi ya Super8.
Mkongwe huyo aliiambia MAMBO UWANJANI mazoezini hapo jana kuwa anafuraha kusaini mkataba huo na kwamba malengo yake ni kuhakikisha Simba inafika mbali katika ligi ya nyumbani na kimataifa kama ilivyo desturi yake.
Kibadeni aliyewahi kuifikisha Simba kwenye fainali ya michuano ya CAF mwaka 1993 ambapo walifungwa 2-0 dhidi ya Stella Abidjan, alisema kitu cha muhimu anachopenda ni kupewa muda ili afanye kazi zake.
"Nimetua rasmi Simba kwa mkataba wa miaka miwili na matarajio yangu ni kuifikisha mbali. Mashabiki watarajie lolote katika michuano ya Kagame kutokana na muda mfupi uliopo, lakini katika ligi wasiwe na shaka," alisema.
Aliongeza anachopenda kwa uongozi wake ni kupewa nafasi ya kufanya kazi bila kuingiliwa ili mwisho iwe rahisi kwao kumbana.
"Hakuna jambo ambalo silipendi kama kuingiliwa kazini, kila mtu atekeleze majukumu yake. Benchi la ufundi tuachwe tuifanye kazi na wataona nini tutakachokifanya kwani najiamini naweza," alisema Kibadeni.
Kuhusu wachezaji waliosimamishwa na uongozi kwa tuhuma za utovu wa nidhamu, Kibadeni alisema hawana nafasi kwake kwa kuwa siku zote yeye amekuwa muumini wa suala la nidhamu kwa wachezaji.
"Kama viongozi waliwasimamisha kwa utovu wa nidhamu, kwangu pia hawana nafasi ili wasije wakaniharibia kazi, nitafanya kazi na wachezaji wote walio tayari kuitumikia Simba kwa hali na mali ili ifike mbali," alisema.
Makocha wasaidizi waliompokea Kibadeni, Jamhuri Kihwelu 'Julio', Seleman Matola na Amri Said walisema wamefurahia ujio wa mwalimu huyo aliyewahi kuwanoa enzi za uchezaji na kuamini benchi la ufundi sasa limekamilika na Simba itatisha.
"Simba ijayo itatisha, nani asiyemjue Super Coach King Kibadeni, hebu piga picha huku King, hapa Julio aaah Simba itatakata tuombe Mungu, ila tumefurahi mno kurejeshwa kwa Kibadeni Msimbazi," alisema Julio.
Katika hatua nyingine jumla ya wachezaji 11, wakiwamo watano kutoka nje ya nchi jana walijitokeza kwenye majaribio ya kuwania kusajiliwa Simba yaliyosimamiwa na makocha wa Simba akiwamo kocha mkuu Kibadeni.
Wachezaji hao kutoka DRC ni Fabian Tshayaz, Fabrice Balou na Patrick Milambo wote kutoka klabu ya AS Vita na Joe Fils kutoka Le Verez Club.
Wengine waliojitokeza kuomba kazi Msimbazi ni Mohammed Abdallah aliyekuwa anachezea Ferreviario De Nampula ya Msumbiji, Adeyun Saleh wa Miembeni Zanzibar na wanaotokea Dar es Salaam, Shaaban Kondo (Mbagala Scalet Academy), Ramadhani Kipicha (Buza) na Shaaban Said (Boom FC ya Ilala).