AZAM YAMALIZANA NA STRAIKA WAKE
Klabu ya Azam imemwongezea mkataba mshambuliaji wao wa kimataifa
kutoka Kenya, Humprey Mieno baada ya kumaliza kuitumikia klabu hiyo kwa
mkopo akitokea Sofapaka ya Kenya.
Mieno ambaye alionyesha kiwango kizuri wakati wa
Ligi Kuu na kuifanya Azam kubaki katika nafasi ya pili, kulimfanya kocha
wa Azam kuuomba uongozi kumpatia mkataba mchezaji huyo.
Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo ambaye hakutaka
jina lake kuandikwa, alithibitisha kumalizika kwa makubaliano kati ya
mchezaji na uongozi wa Azam na kufikia mwafaka.
“Mieno alikuwa mmoja wa wachezaji waliomaliza
mkataba, lakini kocha pamoja na uongozi umeona ni vyema ukampa muda
zaidi kwani ameonyesha kiwango kizuri,”alisema kiongozi huyo.
Kwa upande wa rais wa Sofapaka Elly Kalekwa,
alisema kiungo huyo amefikia mwafaka na klabu ya Azam baada ya
kumwongezea mkataba na wao tayari wamepokea barua ya makubaliano.
Kalekwa alisema Mieno ameonyesha uwezo mkubwa ndani ya kikosi cha Azam ndiyo sababu iliyosababisha kuongezewa mkataba.
“Hatutakuwa na Mieno tena baada ya Azam
kumwongezea mkataba, na sisi kama viongozi wake tunamtakia heri na
mafanikio katika kazi,”alisema Kalekwa.