AKINA MBIYAVANGA WAONDOLEWA TENA NA KIBADEN SIMBA
Kocha mpya wa timu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Abdallah 'King' Kibadeni
Wachezaji hao ambao Kibadeni na wasaidizi wake hawajaridhishwa na viwango vyao ni Fabrice Baloko, Fabian Tshiyaz, Patrick Milambo na Joe Fills.
Akizungumza na mtandao huu Kibadeni ambaye aliiongoza Simba kufikia fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, alisema kuwa bado amewapa nafasi wachezaji wengine wawili, kiungo mkabaji kutoka Ivory Coast, Kouakou Martial na beki anayetoka Nigeria, Youssouf Gabra.
Aliongeza kuwa bado milango iko wazi katika kuangalia wachezaji wa kuwasajili na jana jioni zaidi ya nyota watatu kutoka klabu za Prisons, JKT Ruvu na JKT Oljoro, walitarajia kuanza mazoezi chini ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba.
Kocha huyo alisema kwamba anataka kufanya usajili kwa umakini ili kuhakikisha msimu ujao Simba inafanya vizuri na anarejesha imani kwa mashabiki wake.
Kocha huyo mkongwe alisema kuwa kikosi hicho ambacho kiko katika mabadiliko kinahitaji muda ili kuweza 'kusimama' na kucheza kama timu hasa kufuatia uamuzi uliofanyika wa kujenga upya timu yenye mchanganyiko wa wachezaji chipukizi na wazoefu.
"Timu hii ina wachezaji wakubwa ambao wanatakiwa kuelimishwa na kubadilishwa kidogo na wachezaji vijana nao wanahitaji kuelimishwa ili kujua nini wanatakiwa kufanya kukabiliana na ushindani," alisema kocha huyo.
Aliongeza kwamba kikubwa anachokiangalia yeye ni wachezaji kuwa na nidhamu huku akisisitiza kutowarudisha wachezaji waliosimamishwa kwa kosa la utovu wa nidhamu.
Simba tayari imeshawasajili Issa Rashid kutoka Mtibwa, Zahor Pazi (Azam), Andrew Ntalla (Kagera Sugar), Ibrahim Twaha (Coastal Union) na Mganda Samuel Ssenkoomi wa URA ya Uganda.
Wakati huo huo, Simba inatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa Juni 12 mwaka huu dhidi ya Sofapaka inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Kenya.
Mratibu wa mchezo huo,George Wakuganda, alisema kuwa mchezo huo utatumiwa na Simba kutambulisha wachezaji wapya.