Aisha Masaka arejea Brighton
Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Aisha Masaka, amerejea rasmi kikosini na kuanza mazoezi na wachezaji wenzake wa klabu ya Brighton & Hove Albion ya nchini Uingereza kufuatia kupona majeraha makubwa ya goti yaliyomweka nje ya uwanja kwa muda mrefu tangu mwaka 2025.
Mshambuliaji huyo tayari yupo nchini Uingereza akifanya programu za uwanjani zinazolenga kumpa utimamu wa mwili na kurejesha kiwango chake cha ushindani kabla ya kurejea rasmi kwenye michezo ya kimashindano.
Kurejea kwake kumeleta matumaini makubwa kwa benchi la ufundi la Brighton pamoja na timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, ambazo zote zinanufaika na uwezo wake wa kupachika mabao.
Hatua hii ni pigo lililogeuka kuwa furaha, ikizingatiwa kuwa majeraha hayo ya goti yalimnyima fursa ya kushiriki mashindano makubwa ikiwa ni pamoja na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON). Kurejea kwake uwanjani kunatajwa kuwa msukumo mpya katika ushindani wa nafasi ya kikosi cha kwanza ndani ya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini Uingereza (WSL).
