Singida Black Stars balaa, yamrudisha mfungaji bora msimu uliopita
Singida Black Stars imekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Jean-Charles Ahoua, kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kuondoka CR Belouizdad ya Algeria kama mchezaji huru.
Taarifa za usajili huo zinaeleza kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 atakuwa sehemu ya kikosi cha Singida kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Kagame.
Ahoua anarudi Tanzania miezi michache baada ya kuondoka Simba SC, ambako aling'ara kwa kiwango bora na kuwa mmoja wa viungo waliovutia zaidi katika Ligi Kuu Bara kabla ya kuhamia CR Belouizdad mapema mwaka huu.
Usajili huo unatajwa kuwa nyongeza kubwa kwa Singida Black Stars, ambao wanaendelea kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya mashindano ya ndani na kimataifa.
Mashabiki sasa wanasubiri kumuona Ahoua akianza rasmi maisha mapya akiwa na jezi ya Singida Black Stars kwenye michuano ya Kagame Cup.
