Mpishi wa mabao Afrika Kusini atambulishwa Simba

Klabu ya Simba imemtambulisha rasmi kiungo mshambuliaji wa Sekhukhune United Keletso Makgalwa, ambaye ameonekana kuwa mmoja wa wachezaji hatari zaidi wa kutengeneza nafasi za mabao katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini ndani ya misimu miwili iliyopita.

Makgalwa, mwenye umri wa miaka 29 amejijengea sifa kubwa Sekhukhune United kutokana na kasi yake, uwezo wa kupiga chenga na hasa ubora wake wa kutoa pasi za mwisho zinazozaa mabao.

Msimu wa 2024/25 Makgalwa alikuwa mchezaji aliyeongoza kwa pasi za mabao (assists) kwenye ligi kuu ya Afrika Kusini baada ya kutoa asisti 11 katika mechi 28 za ligi na alifunga mabao sita katika
mashindano yote na kumaliza msimu akiwa miongoni mwa wachezaji walioteuliwa kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Ubora wake haukuishia hapo katika msimu wa 2025/26, Makgalwa aliendelea kuwa miongoni mwa wachezaji wanaotengeneza nafasi nyingi za mabao, akichangia asisti saba kwenye ligi, huku akiendelea kuwa silaha muhimu ya Sekhukhune United katika eneo la ushambuliaji.

Nyota huyo aliwahi kuwa mchezaji wa Mamelodi Sundowns kwa kipindi cha 2018 hadi 2024 baada ya kupandishwa kutoka akademi ya klabu hiyo kabla ya kutolewa kwa mkopo kuzitumikia timu nyingine za Afrika
Kusini.