Tumepanga kuwashambulia Yanga- Ndayiragije
Kocha Mkuu wa TRA United SC, Etienne Ndayiragije, ameweka wazi kuwa mchezo wao ujao dhidi ya mabingwa watetezi, Young Africans SC, utakuwa ni fursa adhimu ya kuendelea kuitangaza na kuitambulisha timu yao kwa Watanzania.
Ndayiragije amebainisha kuwa tofauti na mechi ya mzunguko wa kwanza iliyopigwa kwenye uwanja wao wa nyumbani jijini Arusha na kumalizika kwa sare ya 0-0, mchezo wa kesho utakuwa wa aina yake kwani unachezwa katika Uwanja wa KMC huku kikosi chake kikiwa kimeshapata mdundo mzuri wa ushindani.
Katika upande wa mbinu, kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa amefunguka mpango madhubuti wa kukabiliana na safu kali ya ushambuliaji ya Yanga SC, akisisitiza kuwa hawatenda kuzuia badala yake wataingia kwa kushambulia zaidi ili kuwalazimisha wapinzani wao kurudi nyuma kulinda lango lao.
Aidha, Etienne Ndayiragije amepiga chini dhana kuwa timu hiyo ni tishio wakiwa tu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, akitolea mfano matokeo yao makubwa ya ugenini ikiwemo ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Singida na ushindi mwingine mbele ya KMC, kuashiria kuwa wapo vizuri popote pale.
Kuhusu mustakabali wao kwenye msimamo, Ndayiragije ameweka kadi zote mezani kwa kufafanua kuwa tangu walipopanda daraja, klabu hiyo haijawahi kuwa na malengo ya kumaliza kwenye nafasi nne za juu (Top Four) au kukata tiketi ya kwenda kimataifa msimu huu.
Amehitimisha kwa kusema kuwa lengo kuu la TRA United kwa sasa ni kuonyesha soka safi, la kiushindani na kuitangaza taasisi yao ya TRA vizuri kupitia mchezo huo wa kiwango cha juu.
