Wachezaji saba wa Eritrea watokomea Eswatini
Wachezaji saba kutoka kikosi cha soka cha Eritrea kilichopata ushindi wa kihistoria nchini Eswatini wiki iliyopita hawajarejea nyumbani.
Wakati baadhi ya wachezaji wenzao walirejea kutoka Afrika Kusini, jirani wa Eswatini, inadaiwa kuwa wachezaji hao saba wametoweka.
Kumekuwa na matukio kadhaa katika miaka ya hivi karibuni ambapo raia wa Eritrea wanaoshiriki michezo mbalimbali hawajarejea nyumbani baada ya mashindano ya kimataifa.
Makundi ya haki za binadamu yameelezea serikali ya Asmara kuwa ni yenye ukandamizaji mkubwa — tuhuma ambazo mamlaka zimekuwa zikizikanusha. Licha ya kuwa na idadi ndogo ya watu, mamia ya maelfu ya Waeritrea wamekimbilia kuomba hifadhi nje ya nchi.
Habari za kutoweka kwa wachezaji hao ni pigo kwa timu hiyo, ambayo baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Eswatini na ushindi wa jumla wa 4-1, ilikuwa ikisherehekea kurejea katika hatua ya makundi ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 19.
Kati ya kikosi cha wachezaji 24, ni wachezaji 10 pekee waliokuwa wanaishi Eritrea, na kati yao ni watatu tu — akiwemo nahodha wa timu Ablelom Teklezghi — ambao hadi sasa wamerejea nyumbani,.
