Nyota wa timu ya taifa ya Uganda na klabu ya Vipers SC, Allan Okello, amekamilisha uhamisho wake kwenda Young Africans SC (Yanga) kwa ada inayoripotiwa kufikia dola 300,000 (takriban Sh bilioni 1 za Uganda).
Uhamisho huo unamfanya Okello kuwa mchezaji wa pili kwa gharama kubwa zaidi kuwahi kuuzwa na Vipers SC, nyuma ya Farouk Miya aliyenunuliwa na Standard Liège kwa dola 400,000 mwaka 2016.
Kwa mujibu wa NBS Sport, ada hiyo pia imepita ile ya Cesar Manzoki aliyesajiliwa na klabu ya China kwa dola 200,000.
Okello mwenye umri wa miaka 25 amesaini mkataba wa miaka mitatu na Yanga, akihitimisha harakati za muda mrefu za mabingwa hao wa Tanzania kumuwania.
Awali, Vipers waliwahi kukataa ofa kubwa zaidi ya dola 500,000 kutoka Yanga mwanzoni mwa msimu wa 2025/26, wakitaka kumbakiza Okello kwa ajili ya kampeni ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hata hivyo, baada ya kushindwa kufuzu hatua ya makundi na Okello kubaki na mwaka mmoja wa mkataba bila nia ya kuongeza, klabu ililazimika kufanya uamuzi mgumu wa kumuuza Okello.
