TIMU ya Simba SC imepoteza mechi ya pili mfululizo ya Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa mabao 2-1 na wenyeji, Stade Malien usiku huu Uwanja wa Machi 26 Jijini Bamako nchini Mali.
Mabao ya Stade Malien yamefungwa na mshambuliaji Mcameroon, Taddeus Nkeng dakika ya 16 na beki mzawa, Ismaila Simpara dakika ya 23, wakati bao pekee la Simba limefungwa na kiungo wa Afrika Kusini, Neo Maema dakika ya 54.
Kipa wa Simba SC, Yakoub Suleiman Ali alipangua mkwaju wa penalti wa Mcameroon Taddeus Nkeng dakika ya 62, kabla ya kiungo Msenegal wa Wekundu hao wa Msimbazi, Alassane Kante kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 82.
Kwa ushindi huo, Stade Malien inafikisha pointi nne sawa na Petro de Luanda ya Angola timu hizo zikilingana hadi wastani wa mabao baada ya mechi za mwanzo, zikifuatiwa na Espérance de Tunis yenye pointi mbili na Simba SC inaendelea kushika mkia baada ya kupoteza mechi zote mbili za mwanzo.
Ikumbukwe mechi ya kwanza Simba SC ilifungwa 1-0 na Petro de Luanda ya Angola Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam, wakati Stade Malien ililazimishwa sare ya bila mabao na Espérance Uwanja wa Hammadi Agrebi, Tunisde Jijini Tunis nchini Tunisia.
