MABINGWA watetezi, Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Pongezi kwa wafungaji wa mabao ya leo – wachezaji wapya, beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliyesajiliwa kjutoka kwa watani, Simba SC dakika ya 38 na kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Chad, CĂ©lestin Ecua aliyesajiliwa kutoka Zoman FC ya Ivory Coast dakika ya 83.
Baada ya mchezo huo, Tshabalala ambaye anafahamika pia kwa jina lingine la utani, Zimbwe Junior alikabidhiwa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi kwa kiwango kizuri alichokionyesha leo.
Kwa ushindi wa leo, Yanga inafikisha pointi saba katika mchezo wa tatu baada ya kuichapa Pamba Jiji mabao 3-0 kwenye mchezo wa kwanza na sare ya bila mabao na Mbeya City kwenye mchezo uliofuata Jijini Mbeya.
Kwa upande wao Mtibwa Sugar waliorejea Ligi Kuu msimu huu baada ya msimu mmoja wa kucheza Championship wanabaki na pointi zao tano za mechi tano sasa kufuatia kushinda mechi moja awali, kufungwa moja na sare mbili.
