TIMU ya Yanga imefanikiwa kwenda Hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Silver Strikers ya Malawi jioni hii Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga SC leo yamefungwa na beki Dickson Nickson Job dakika ya sita na kiungo Muivory Coast, Peodoh Pacome Zouzoua dakika ya 34.
Kwa matokeo hayo, Yanga wanatinga hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla wa 2-1 kufuatia kufungwa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Jumamosi iliyopita katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Pili Uwanja wa Taifa wa Bingu Jijini Lilongwe nchini Malawi.
Bao pekee la Silver Strikers siku hiyo lililoizamisha Yanga lilifungwa na kiungo mshambuliaji Andulu Yosefe dakika ya 76 akimalizia kazi nzuri ya kiungo Uchizi Vunga.
Droo ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika itapangwa Jumatatu ya Novemba 3 katika studio za SuperSport Jijini Johannesburg, Afrika Kusini ambao ni washirika wa Matangazo wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuanzia Saa 7:00 mchana.