Na Prince Hoza Matua
WANAYANGA wanataka timu yao icheze mpira wa kupigiana pasi fupi fupi kwa staili ya kwenda mbele, hawataki mpira wa taratibu na kupigiana pasi za kurudi nyuma, wameshazoeshwa na makocha wao waliopita.
Tunajua kabisa kwamba Wanayanga kupata ushindi kwao sio habari ngeni, wamezoeshwa na makocha waliopita, Yanga kushinda makombe ni jadi yao wala sio kitu kigeni, vitu ambavyo kwao ni vigeni ni pale timu yao inafungwa au kutoka sare.
Kwa kifupi mashabiki wa Yanga sio watu wa mpira, hawajui kanuni za mpira, kwamba kuna matokeo aina tatu tu, kufungwa, kushinda na kutoka sare, lakini mashabiki wa Yanga wanajua tokeo moja tu la kushinda.
Ikitokea timu yao imetoka sare, kocha ananyooshewa kidole, kama sare ya kwanza wanamvumilia kama ya pili wanampa kalipio kali na kama ya tatu wanamfungashia virago, kwa kifupi hawataki matokeo ya aina mbili yatokee.
Lakini kwa sasa mashabiki wa Yanga wamebadilika kidogo, kushinda wamegeuza kama asilia yao, ila wanataka timu yao icheze kwa ku- press kwa staili ya kwenda mbele, Nasreddine Nabi alikuja na staili ya pasi fupi fupi kwa kurudi nyuma.
Enzi zake Nabi mchezaji Salum Abunakar "Sureboy" alipata nafasi kwenye kikosi chake, Sureboy aliyesajiliwa kutoka Azam FC aling' ara sana kwenye kikosi hicho, nakumbuka Sureboy alimsaidia sana Feisal Salum Feitoto.
Sureboy alichangia kumshawishi Feitoto kuipenda mchezo wa soka na hata walipokutana Yanga, kiungo huyo ambaye sasa anakipiga Azam FC alimshukuru sana na kueleza historia yake.
Nabi akiwa Yanga aliisaidia kutinga fainali kombe la Shirikisho Afrika na pia kutwaa makombe yote matatu, kwa maana Ligi Kuu bara, kombe la FA na Ngao ya Jamii, kwa kifupi historia ya Yanga kutawala mpira wa Tanzania ulianzia kwa Nabi.
Lakini baadaye Nabi aliondoka na kujiunga na FAR Rabat ya Morocco, akaja Miguel Gamondi, wengi hawakuujua ubora wa kocha huyo raia wa Argentina.
Gamondi likuja na falsafa yake ya soka la pasi fupi kwa kwenda mbele, Gamondi alikuwa muumini wa kushambulia kwa spidi na hapo ndipo Yanga ilipoambukizwa ubaya hadi Simba wakaja na neno ubaya ubwela.
Gamondi aliendeleza mazuri ya Nabi, kwani kikosi cha Yanga kilitetea Mataji yake na vile vile kufika robo fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika, Yanga ilikuwa tishio ndani na nje ya nchi, Gamondi naye aliondolewa baada ya timu yake kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Azam FC na Tabora United.
Alipoondoka Gamondi akaletwa Sead Ramovic raia wa Ujerumami, Ramovic aliendeleza mazuri ya mtangulizi wake Gamondi na timu ikazidi kusifika, gusa achia twende kwao ilisikika ndani ya Yanga huku mashabiki wake waliendelea kifurahia.
Hata hivyo Ramovic aliondoka baada ya kupata timu Algeria, lakini Yanga walimchukua Miloud Hamdi raia wa Algeria na akaja kuendeleza yale yale ya wenzake, Nabi, Gamondi na Ramovic.
Miloud naye akaondoka mitaa ya Jangwani, wakamleta Ramon Folz, maisha ya Folz ndani ya Yanga sio mazuri, mashabiki hawafurahishwi na mfumo wa uchezaji, kwani amebadilisha kila kitu na timu haichezi tena kwa ku- press na pia haijulikani wanacheza kwa staili gani.
Kelele zimezagaa kama abiria wa mwendokasi wa Kimata mpaka Mkuu wa Mkapa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kuwatembelea, Wanayanga kikubwa wao wanataka gusa achia twende kwao, Folz badalika.
ALAMSIKI
+255766 514 040