TIMU ya taifa ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars leo imefanikiwa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika Wanawake 2026 nchini Morocco baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji, Ethiopia jioni ya leo Uwanja wa Taifa wa Dire Dawa mjini Dire Dawa katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Pili na ya mwisho ya mchujo.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, kiungo mshambuliaji wa Trabzonspor ya Uturuki, Diana Lucas Msewa na kwa matokeo hayo Tanzania inafuzu WAFCON ya mwakani kwa ushindi wa jumla wa 3-0 kufuatia ushindi wa 2-0 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam – mabao ya washambuliaji Aisha Juma Mnunka wa Simba Queens dakika ya 23 na Jamila Rajab Mnunduka wa JKT Queens dakika ya 56.
Inakuwa mara ya tatu kwa Twiga Stars kufuzu Fainali za WAFCON baada ya mwaka 2010 nchini Afrika Kusini na 2024 nchini Morocco na mara zote walitolewa katika hatua ya makundi.
